• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 9:37 AM
DIMBA PWANI: Moyeni United FC yaendelea kukua

DIMBA PWANI: Moyeni United FC yaendelea kukua

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

HAKUNA sehemu yoyote ya mashinani ya ukanda wa Pwani ambayo inakosa kuwa na timu yenye wachezaji wenye tajriba ya kusakata soka ya hali ya juu.

Katika kijiji cha Moyeni cha Kaunti ya Kwale, kuna timu ya jina la kijiji hicho ya Moyeni United FC ambayo ina wanasoka kadhaa ambao wakipata nafasi, wanaweza kuchezea timu zenye majina makubwa Pwani ikiwemo ile ya Ligi Kuu ya Bandari FC.

Moyeni United FC imekuwa ikiwika katika eneo la wadi ya Kinango na mwaka huu wa 2020, imeweza kubeba mataji mawili ya Mtili Cup na Itambo Cup, vikombe vilivyodhaminiwa na wale wanaotaka kupigania kiti cha Mwakiklishi wa wadi hiyo uchaguzi wa mwaka 2022.

Vijana wa moyenbi United wakifanya mazoezi kujitayarisha kwa mechi zao zijazo. Picha/ Abdulrahman Sheriff

“Tunafurahikia kuona vijana wa sehemu yetu hii wanachukulia soka kuwa na umuhimu huku wakijitahidi kuhakikisha wanafika mbali n ahata kufika kushiriki ligi kuu ya hapa nchini,” amesema mfadhili wa klabu hiyo, Abdalla Ali Nzala.

Nzala anasema wanafanya bidii kuhakikisha timu hiyo inapata fursa ya kushiriki katika Ligi ya Kaunti ya Kwale lakini changamoto kubwa ni ukosefu wa ufadhili kwani ligi ama mashindano ya vikombe yana mahitaji mengi.

Nzala amesema kuwa Moyeni United inayopewa mafunzo na Kocha Mkuu, Roy Madonga na naibu wake Rama Kalama, ina timu tatu ambazo ni za vijana wa umri chini ya miaka 15, yazaidi ya miaka 15 na ya tatu ni ya soka ya wanawake ambayo ndiyo inaanzishwa.

“Tumeanzisha timu hiyo ya soka ya wasichana kwa sababu tunataka wasichana wetu nao wasiachwe nyumba kwani katika sehemu nyingi za Pwani, timu za wasichana ziko na zinapiga hatua ya kujiendeleza,” akasema Nzala.

Mfadhili wa Moyeni United FC Abdalla Ali Nzala. Picha/ Abdulrahman Sheriff

Kocha Madonga alisema kuwa timu zake mbili hizo za wavulana zimeimarika na ziko tayari kushiriki kwenye mashindano yoyote huku akitamba kuwa kikosi chake chipukizi wa umri chini ya miaka 15, kimekuwa mwiba kwa timu za eneo la Kinango.

“Hawa vijana wa umri chini ya miaka 15 imekuwa ikiwapendeza mashabiki wa kandanda katika eneo la Kinango na nina imani kubwa muda wa miaka miwili ijayo, vijana hao wakipanda ngazi, wataweza kutisha timu nyingine,” akasema mkufunzi huyo.

Nzala alishukuru serikali ya Kaunti ya Kwale kwa kuwasaidia kuwalimia kiwanja, kuwapa neti za magoli na kila mwaka kupatiwa mipira pamoja na jezi.

“Tunaamini serikali yetu inazingatia michezo kuwa na umuhimu na hivyo vijana wajitokeze wapate kusaidika,” akasema.

Baadhi ya mashabiki wa soka wa sehemu hiyo wanasema wangefurahia kama klabu kubwa kutoka Mombasa na sehemu nyingine za Pwani zingekuwa zikifika hapo kucheza mechi za kirafiki ambapo vijana wao watapata uzoefu wa haraka.

“Nina hakika kama timu zikiwemo za Bandari, Modern Coast Rangers, Congo Boys na Coast Stima zitakuwa zikifika hapa kwetu, wachezaji wetu watapata uzoefu wa haraka wa kucheza soka ya kupendeza zaidi ya ilivyo wakati huu,” amesema shabiki Omari Muhamadi.

Shabiki mwingine, Stephen Solomon amesema kuna umuhimu wa wakazi wa sehemu hiyo kuwa karibu na wachezaji kwani kunaweza kuwasaidia vijana hao kufika mbali kisoka.

“Nakumbuka zama zetu huko Mombasa, mashabiki wa Feisal na Liverpool (Mwenge) walikuwa wakifika mazoezini kuwa motisha wanasoka wao na ilikuwa ikiwasaidia kuinua vipaji vyao,” akasema Solomon.

You can share this post!

Ibrahimovic afunga mawili na kusaidia AC Milan kuzamisha...

Lukaku na Sanchez wasaidia Inter Milan kutoka nyuma na...