Diogo Jota afunga matatu Liverpool wakidhalilisha Atalanta 5-0 katika UEFA
Na MASHIRIKA
NYOTA Diogo Jota alifunga mabao matatu na kuwezesha Liverpool kuwapepeta Atalanta kutoka Italia 5-0 ugenini kwenye mechi ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Novemba 3, 2020.
Chini ya kocha Jurgen Klopp, Liverpool ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) sasa wameibuka washindi wa mechi zao zote tatu za UEFA kwenye Kundi D bila ya kufungwa bao.
Kikosi hicho sasa kinahitaji ushindi mmoja pekee katika mechi zilizosalia kundini ili kujikatia tiketi ya kuingia hatua ya 16-bora.
Jota ambaye alisajiliwa na Liverpool mwanzoni mwa msimu huu kutoka Wolves alizidi kudhihirisha kwamba ndiye anayestahili kutwaa kabisa nafasi ya Roberto Firmino katika safu ya mbele ya kikosi cha Klopp.
Fowadi huyo raia wa Ureno alifungua ukurasa wake wa mabao katika dakika ya 16 kabla ya kufunga mengine kunako dakika za 33 na 54. Magoli mengine ya Liverpool dhidi ya Atalanta yalifumwa na Mohamed Salah na Sadio Mane mwanzoni mwa kipindi cha pili. Watatu hao walimtatiza pakubwa kipa wa Atalanta, Marco Sportiello.
Liverpool waliotumia mchuano huo kumkaribisha kipa Alisson Becker kutoka mkekani, walikosa huduma za nyota Fabinho na Virgil van Dijk wanaouguza majeraha.
Katika mechi nyingine ya Kundi D, miamba wa soka wa Uholanzi, Ajax, walisajili ushindi wao wa kwanza kwa kuwapokeza Midtjylland kichapo cha 2-1. Kikosi hicho cha Denmark sasa kinavuta mkia wa kundi bila alama yoyote.
Liverpool wametinga fainali ya UEFA mara mbili katika kipindi cha misimu mitatu iliyopita. Waliambulia nafasi ya pili mnamo 2018 baada ya kuzidiwa maarifa na Real kwenye fainali kabla ya kuwaangusha Tottenham Hotspur mnamo 2019 na kutwaa ufalme wa taji hilo kwa mara ya sita katika historia.
Ushindi wa 5-0 uliosajiliwa na Liverpool ndio mnono zaidi kwa kikosi cha Uingereza kuwahi kuvuna dhidi ya mpinzani kutoka Italia kwenye soka ya UEFA.