DOHA: AK yakana dai baadhi ya wanariadha wanatumia pufya
Na CHRIS ADUNGO
SHIRIKISHO la Riadha la Kenya (AK) limekanusha madai kwamba baadhi ya watimkaji wa Kenya wanaojiandaa kwa Riadha za Dunia zitakazoandaliwa jijini Doha, Qatar kati ya Septemba 27 na Oktoba 6, 2019, wameshiriki matumizi ya dawa za kusisimua misuli.
Katika taarifa yake, AK imepuuzilia mbali tetesi hizo na kusisitiza kwamba zimetolewa katika kipindi hiki ili kupaka tope jina la Kenya miongoni mwa mataifa wanachama wa Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) na kuibua hofu isiyostahili miongoni mwa washiriki na mashabiki wa mbio hizo kwa lengo la kuwapotezea dira wanariadha wa humu nchini.
“Wanariadha wote watakaowakilisha Kenya walitimiza masharti ya AK na IAAF. AK haifahamu mwanariadha yeyote katika kambi ya Team Kenya aliyetumia pufya. Itakuwa vyema iwapo m atatuwasilishia ushahidi wake au hata kuwapokeza vinara wa AIU,” akasema Rais wa AK, Jackson Tuwei kwa kusisitiza kwamba ni Shirika la Kitaifa la Kukabiliana na matumizi ya pufya humu nchini (ADAK) pekee ndilo lenye mamlaka ya kuwakagua wanaridha wala si AK.
Mwanzoni mwa wiki hii, runinga ya ZDF ya Ujerumani kupitia kwa mwanahabari Harm, ilidai kwamba kuna uozo mkubwa wa matumizi ya pufya miongoni mwa wanariadha wa Kenya wanaojizatiti kwa mbio za Doha.
Mkuu wa Kitengo cha Maadili (AIU) katika Shirikisho la IAAF, Brett Clothier alisema kuwa Kenya huenda ikapigwa marufuku iwapo runinga ya ZDF iliyo na makao mjini Mainz itawapokeza ushahidi wa kuwa wanariadha wengi wa Kenya wanatumia dawa aina ya EPO kwa nia ya kusisimua misuli.
“Haya ni madai ya kutisha na huenda yana chembechembe za ukweli kwa sababu matatizo hayo na ufisadi si mambo mageni Kenya. Tupo radhi kupokea ushahidi na kuchunguza madai ya visa hivi,” Clothier alinukuliwa na runinga hiyo akisema kwamba Kenya ni miongoni mwa mataifa matano yanayoongoza kwa matumizi ya pufya.
“Ipo video ya mwanariadha mmoja mwanamume na mwingine mwanamke walionaswa na kamera zilizofichwa wakidungiwa EPO kwenye mishipa yao,” runinga hiyo ilisema.
Wanariadha
Iliongeza kuwa ilizungumza na daktari mmoja ambaye hakutaka kutajwa aliyedai kuwa alikuwa na wanariadha wanane katika timu ya taifa ya sasa.
Kulingana na ZDF, kiini cha uovu huo nchini Kenya ni ufisadi unaoendelezwa na AK na ADAK.
“ADAK na AK wanaficha matokeo ya wanariadha kadhaa ili wasipigwe marufuku. AK na ADAK zinashirikiana ili kuvuna pakubwa kutokana na mpango huo unaowalenga wanariadha na mameneja wenye kiu ya kupata mafanikio kupitia njia za mkato,” ikasema ZDF.
Mnamo 2015 na 2016, Kenya itakayowakilishwa na wanaridha 50 nchini Qatar iliponea chupuchupu kupigwa marufuku katika Olimpiki na mashindano mengine makubwa ya riadha kutokana na madai ya watimkaji kutumia pufya. Jijini Doha, Kenya itawakilishwa na karibu wanariadha 50.