Michezo

DOHA: Macho kwa Obiri

September 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

NYOTA Hellen Obiri, Agnes Tirop na Rosemary Wanjiru watakabiliwa na mtihani mkali katika kampeni zao za kushindia Kenya medali katika mbio za mita 10,000 kwenye Riadha za Dunia zinazoingia siku ya pili leo Jumamosi jijini Doha, Qatar.

Obiri, ambaye ni malkia wa Afrika, Jumuiya ya Madola na Dunia katika mbio za mita 5,000, ni mmoja wa watimkaji ambao Kenya inategemea kupata medali katika mbio hizi za kuzunguka uwanja mara 25.

Imani ya Wakenya kwake hasa inatokana na kubobea mwaka huu akishinda mbio za kilomita 10 kwenye Mbio za Nyika za Dunia pamoja na kumaliza wa pili nyuma ya Tirop katika mbio za kitaifa za mita 10,000 jijini Nairobi.

Licha ya kuwa anashiriki mbio za mita 10, 000 kwa mara ya kwanza katika ulingo wa kimataifa, Obiri, 29, anapigiwa upatu kuletea Kenya medali.

Tirop alizoa medali ya shaba miaka miwili iliyopita nchini Uingereza.

Mkimbiaji huyu mwenye umri wa miaka 24 alidhihirisha kuwa yuko katika hali nzuri alipofyatuka katika mbio za mita 5,000 kwa dakika 14:20.68 jijini London mnamo Julai na kuingia katika nafasi ya sita kwenye orodha ya wakimbiaji walio na kasi ya juu duniani.

Rosemary Wanjiru (31:11.79), ambaye kabla ya mbio za kuchagua timu ya Kenya hakuwa anajulikana, anakamilisha wawakilishi wa Kenya hapa.

Raia wa Uholanzi Sifan Hassan ni mmoja wa wakimbiaji matata ambao Wakenya watalazimika kufanya kazi ya ziada ili kumzima.

Mzawa huyu wa Ethiopia amekuwa na fomu ya kutisha mwaka huu aking’aa katika mbio za mita 1,500 hadi nusu-marathon na kufanya nchi yake kumchagua kuhangaisha katika vitengo vitatu, zikiwemo mbio za mita 10,000.

Ethiopia inawakilishwa na wakali Tsehay Gemechu, Senbere Teferi, Letesenbet Gidey na Netsanet Gudeta.

Mshindi wa makala yaliyopita Almaz Ayana kutoka Ethiopia hatatetea taji lake baada ya kufanyiwa upasuaji mara mbili kwenye goti lake.

Wakenya Ng’eno Kipng’etich, Emmanuel Korir na Ferguson Rotich watakuwa na kibarua kigumu katika mbio za mita 800 zilizovutia magwiji Nijel Amos (Botswana), Ayanleh Souleiman (Djibouti), Pierre-Ambroise Bosse (Ufaransa) na wakimbiaji kutoka Marekani na Puerto Rico ambao walikuwa na msimu mzuri katika mbio hizi za mizunguko miwili.

Hapo jana, bingwa wa dunia wa mbio za mita 800 Eunice Sum alifuzu kwa hatua ya nusu fainali ya mbio hizo alipomaliza mchujo wa pili katika nafasi ya nne kwa dakika 2:02.17.

Ratiba (mbio ambazo Kenya itashiriki): Mita 800 (mchujo wa wanaume, 5.15pm), mita 800 (nusu-fainali ya wanawake, 7.15pm), Mita 4×400 kupokezana vijiti (mchujo wa mseto, 8.00pm), Mita 10,000 (fainali ya wanawake, 9.10pm).