Dua la Arsenal kwa Spurs: Kazieni hao Man City tafadhali!
MASHABIKI wa Arsenal wataomba muujiza wa kipekee Jumanne usiku Tottenham Hotspur watakapoalika Manchester City kwa mechi bab’kubwa itakayoamua nani atakuwa pazuri zaidi kubeba Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) inapotamatika wikendi ijayo.
Man-City wanaendea Tottenham, maarufu Spurs, katika uwanja wa Tottenham Hotspur Stadium jijini London wakijua lazima washinde mchuano huo wa akiba, ili kupiku Arsenal kileleni kabla mechi za raundi ya mwisho kusakatwa kwa mpigo Jumapili ijayo.
Arsenal walirukia tena uongozi wa ligi kwa kufinya wenyeji Manchester United 1-0 mnamo Jumapili usiku.
Bao la fowadi Leandro Trossard dakika ya 20 lilitosha kuwapa Gunners ushindi katika uwanja wa Old Trafford; wakarejea juu ya ligi na alama 86, moja mbele ya Man-City (85) walio na mechi kibindoni.
Man-City watasakata mechi hiyo ya akiba Jumanne dhidi ya Spurs wakijua ushindi huu na wa Jumapili dhidi ya West Ham utawavunia taji la nne mfululizo.
Hakuna timu ambayo imewahi kutimiza hilo katika EPL, hivyo kocha Pep Guardiola na masogora wake watakuwa nari kuandikisha historia.
Aidha, binafsi Guardiola atazoa taji lake la sita la EPL; kumweka sawa na George Ramsey wa Aston Villa na Bob Paisley wa Liverpool enzi zao.
Ni Sir Alex Ferguson (13) wa Man-United pekee ambaye amebeba EPL mara nyingi zaidi kama kocha.
Wachanganuzi data za spoti, Opta, wamedadisi uwezekano wa Man-City kutwaa ubingwa kuwa asilimia 58.7% baada ya kupepeta Fulham 4-0 Jumamosi.
Nao udadisi wa Arsenal umepanda hadi kutoka 23.6% hadi 41.3% kufuatia ushindi wao wa 1-0 dhidi ya Manchester United hapo Jumapili.
Kuelekea mechi ya leo dhidi ya Spurs, kuna uwezekano finyu wa asilimia 45.2 kwa mabingwa watetezi Man-City kutupa alama.
Japo itahitaji nuksi ya kipekee kwani wameingia katika fomu yao kali ya kipindi cha lala-salama kila wanapokuwa usukani mwa EPL.
Tangu sare na Chelsea, masogora wa Guardiola wameshinda mechi 10 kati ya 12 zilizopita ligini wakidondosha alama pekee katika sare na Liverpool na pia Arsenal.
Wameshinda mechi saba mfululizo na hawajaonja kichapo tangu Desemba 6 iliyopita mikononi mwa Aston Villa.
“Tunajua ni vigumu sana lakini tunataka kufanya kitu spesheli,” alisema Guardiola kuhusu azma ya kubeba EPL mara ya nne mfululizo.
Hata hivyo, watahitaji kuruka kamba ya Spurs kwani wamewalemea sana hivi karibuni.
Man-City imeshinda mechi moja pekee kati ya sita zilizopita katika uwanja huo wa Tottenham Hotspur Stadium; mechi ya Kombe la FA msimu huu, lakini haijapata mpenyo katika michuano ya ligi uwanjani humo.
Ni nuksi Guardiola anataka kupunga.
“Tusiposhinda (leo) basi hatutashinda Ligi Kuu. Ni kibarua kigumu kucheza hapa, lakini tunataka kufanya jambo spesheli hivyo lazima tushinde la sivyo Arsenal watakuwa mabingwa,” akahoji.
Mwenyeji wake Ange Postecoglou wa Spurs anatarajia mashabiki wao kuwapa motisha ya ushindi, wala sio kushabikia wageni wao kwa misingi ya kuudhi watani wao wa jadi Arsenal.
“Mashabiki wetu wengi wataleta msisimko wa kutaka tushinde kama ambavyo wamekuwa wakifanya mechi zetu zingine. Ni vigumu kucheza dhidi ya hiki kikosi cha Man-City wakati huu, lakini …(wachezaji wanafahamu) tuna mechi ya kushinda na hilo ndilo tunalenga,” alisema raia huyo wa Australia Jumatatu katika kikao na wanahabari.