Eden Hazard ajeruhiwa tena
NA AFP
MADRID, Uhispania:
Kumbe Real Madrid ilinunua marehemu! Hii inajitokeza baada ya Eden Hazard kupata jeraha tena, huku Real, ambayo ilimnunua Hazard kutoka Chelsea kwa Sh20.9 bilioni mnamo Juni 7 mwaka 2019, ikithibitisha amechanika misuli katika mguu wake wa kulia.
Mshambuliaji huyo Mbelgiji, ambaye anaaminika kupokea mshahara wa Sh55.7 milioni kila wiki uwanjani Santiago Bernabeu, hajachezea Real msimu huu wa 2020-2021 baada pia kukosa kipindi kikubwa cha msimu 2019-2020 akiwa mkekani.
Kusajiliwa kwa Hazard kulipokelewa kwa shangwe na nderemo uwanjani Bernabeu alipotambulishwa mbele ya mashabiki 50,000 hapo Juni 13, 2019.
Hata hivyo, mashabiki walisubiri kwa muda kabla ya kumuona uwanjani akitandaza soka kwa sababu alilalamika kuhisi maumivu mguuni na kisha akaumia wayo katika mechi ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Paris Saint-Germain mwezi Novemba baada tu ya kuanza kuonyesha kilichomfanya kocha Zinedine Zidane atafute huduma zake.
Jeraha la kifundo mwezi Februari 2020 muda mchache baada ya kurejea ulingoni lilishuhudia Hazard akiingia katika chumba cha majeruhi.
Tetesi zilidai mwezi uliopita kuwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29 alirejea mazoezini kwa maandalizi ya msimu mpya akiwa mzito sana.
Hata hivyo, kocha Mfaransa Zidane alimtetea Hazard dhidi ya madai kuwa mchezaji huyo hana weledi na alimjumuisha katika mechi la Ligi Kuu siku ya Jumatano dhidi ya Real Valladolid.
Kabla ya mechi hiyo, Real ilithibitisha kwenye tovuti yake kuwa Hazard amepata pigo hilo jipya. Ingawa mabingwa hao wa Uhispania hawakusema ubaya wa jeraha la Hazard, ripoti zinadai kuwa atakosekana kikosini kwa kati ya wiki tatu na wiki nne.
“Kufuatia vipimo vilivyofanywa na madaktari wa Real Madrid leo (Jumatano), mchezaji Eden Hazard amepatikana na jeraha la kuchanika misuli katika mguu wake wa kulia. Kupona kwake kutaendelea kutathminiwa,” taarifa kutoka Madrid ilisema. Vijana wa Zidane wamezoa alama saba kutoka michuano yao tatu ya kwanza baada ya kucharaza Real Betis 3-2 na kutoka 0-0 dhidi ya Real Sociedad katika mechi mbili za kwanza.
Imetafsiriwa na Geoffrey Anene