Michezo

Elfsborg yavulia kofia beki Joseph Okumu

September 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

KLABU ya Elfsborg inayoshiriki Ligi Kuu nchini Uswidi, imetambua kazi safi ambayo beki Mkenya Joseph Stanley Okumu ameifanyia mwaka 2020 kwa kuchapisha video moja ya mechi alizosakata.

Katika video hiyo ambayo imetundikwa kwenye Twitter (https://twitter.com/AllsvenskanSE/status/1308805132277219329), Okumu, ambaye pia amekuwa akitumiwa kama kiungo, anaonekana akizima mashambulizi, kupokonya wapinzani mpira ama kuokoa mipira hatari.

Video hiyo inaandamana na ujumbe “kiungo Joseph Okumu amekuwa na mwaka wa kufana mwaka huu. Haya hapa mambo makubwa amefanyia Elfsborg uwanjani ambapo amesimamisha wapinzani”.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Kenya mwenye umri wa miaka 23 alijiunga na Elfsborg mnamo Agosti 28 mwaka 2019 kwa kandarasi ya miaka mitatu akitokea Real Monarchs nchini Amerika.

Okumu, ambaye aliwahi kuzichezea Chemelil Sugar, Free State Stars ya Afrika Kusini na AFC Ann Arbor nchini Amerika, amesakatia Elfsborg mechi 15 msimu huu kwenye ligi hiyo ya timu 16.

Elfsborg inashikilia nafasi ya tatu kwa alama 35 kutokana na ushindi nane, sare 11 na vichapo viwili. Iko bega kwa bega na nambari mbili Hacken ambayo ina mechi moja mkononi. Elfsborg na Hacken zilitoka 1-1 Septemba 21 katika mechi ambayo Okumu alikosa kwa sababu ya mafua.