Michezo

Eliud Kipchoge sasa apata herufi za kunogesha hadhi ya jina lake

October 21st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

MSHIKILIZI wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 42, Eliud Kipchoge sasa yuko ligi moja na baadhi ya viongozi wakuu serikalini baada ya kupokea Tuzo ya Heshima ya Elder of the Order of the Golden Heart (E.G.H) Jumapili katika sherehe za kuadhimisha sikukuu ya Mashujaa Dei mjini Mombasa.

Tuzo hii hupeanwa na Rais kwa watu wanaoshikilia nyadhifa za Naibu Rais, Maspika wa Bunge la Kitaifa, Mawaziri, Mama wa Taifa, Mke wa Naibu Rais, Mkuu wa Huduma za Umma na Mkuu wa Vikosi vya Jeshi la Ulinzi.

Mbali na heshima kubwa wamiliki wa tuzo wanao, Kipchoge ataweza kufika katika maeneo ya watu mashuhuri katika uwanja wa ndege bila tatizo na pia kuketi na Waheshimiwa wakati wa sherehe za kitaifa zikiwemo sikukuu za Madaraka (Juni 1), Moi (Oktoba 10), Mashujaa (Oktoba 20) na Jamhuri (Desemba 12).

Tuzo hii, kulingana na Rais wa Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) Jackson Tuwei, haiandamani na zawadi ya kifedha.

Wakenya wengi tu walikuwa wameuliza manufaa ya tuzo ya E.G.H. kwa Kipchoge ni yapi.

Mashujaa Dei ni siku ya kitaifa nchini Kenya, ambayo huadhimishwa Oktoba 20 kila mwaka kutoa heshima kwa watu waliochangia katika kupigania uhuru wa nchi ya Kenya ama waliochangia kuimarika kwa taifa hili baada ya uhuru kupatikana.

Akihutubu mjini Mombasa, Rais Uhuru Kenyatta alitaja Kipchoge kama kielelezo, ambacho Wakenya wanastahili kuiga. Kipchoge ndiye mwanaspoti wa kwanza nchini Kenya kupokea tuzo ya E.G.H.

“Kipchoge alifanya kitu ambacho watu wengi hawakuwahi kufikiria kinawezekana alipokamilisha mbio za kilomita 42 chini ya saa mbili mjini Vienna nchini Austria. Ufanisi wake ulipatikana katika wikendi ambayo bendera ya taifa letu ilipeperushwa vilivyo kote duniani kutokana na kuwa Brigid Kosgei pia alivunja rekodi ya dunia ya marathon ya wanawake siku iliyofuata. Tumebahatika sana kuwa na mkimbiaji kama Kipchoge humu nchini. Yeye ni ametupatia motisha kubwa. Ufanisi huo wake unaonyesha kuwa kupitia uadilifu, bidii na kujitolea tunaweza kufanikiwa katika kila jambo tunataka kufanya. Kwa hivyo, naomba Wakenya wote wafuate mfano wake na kuwa mashujaa katika sehemu wanazohusika,” alisema Rais Kenyatta.

Kipchoge, ambaye ni bingwa wa mbio za kilomita 42 kwenye michezo ya Olimpiki mwaka 2016 pamoja na mataji ya mbio za kifahari za Chicago, London na Berlin, alitimka mbio maalum za INEOS 1:59 Challenge mjini Vienna kwa saa 1:59:40 na kuwa binadamu wa kwanza kukamilisha umbali huo chini ya muda wa saa mbili.

Ufanisi wa Kipchoge, ambaye anashikilia rekodi ya dunia ya marathon ya saa 2:01:39, ulimfanya ajumuishwe katika orodha ya wanariadha 11 kutoka pembe zote za dunia wanaowania Tuzo ya Mwanariadha bora wa mwaka 2019 ya Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF).

Aliibuka mwanariadha bora duniani mwaka 2018.