• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Eliud Kipchoge: Simwamini mtu yeyote… hata kivuli changu

Eliud Kipchoge: Simwamini mtu yeyote… hata kivuli changu

NA LABAAN SHABAAN

Mwanariadha huyo katika mahojiano na BBC Sport Africa, alifichua aliingiwa na kiwewe huku akihofia usalama wake na wa familia yake, baada ya kuhusishwa na kifo cha mshikilizi wa rekodi ya dunia ya Marathon Kelvin Kiptum mnamo Februari 11, 2024.

Kiptum aliaga dunia papo hapo kufuatia ajali ya barabarani, akiwa na kocha wake ndani ya gari.

Bingwa huyo pamoja na kocha raia wa Rwanda Gervais Hakizimana waliangamia kwenye ajali hiyo iliyotokea Kaptagat, Kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Mara baada ya kutangazwa kwa kifo chake Kiptum, baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii walikisia kuwa Kipchoge alikula njama ya kumuua Kiptum ambaye alivunja rekodi yake ya marathon alipokimbia kwa muda wa 2:00:35 mnamo Oktoba 2023 kule Chicago, Amerika.

“Nilishtuka kwamba watu kwenye mitandao ya kijamii wanasema ‘Eliud anahusika katika kifo cha kijana huyu,’” Kipchoge alisema alipohojiwa.

“Hizo zilikuwa taarifa mbaya zaidi kunihusu maishani mwangu. Niliambiwa mambo mengi mabaya… kwamba wangechoma kambi ya mazoezi, wangechoma mali yangu mjini, wangechoma nyumba yangu, wangechoma familia yangu. Haikufanyika lakini hivyo ndivyo ulimwengu ulivyo,” akaongeza.

Ilibidi ampigie mama yake simu kujua kama familia yake ilikuwa salama.

Alihofia maisha ya watoto wake kama wangeenda shuleni na kurudi nyumbani bila kitu kibaya kuwafanyikia.

“Wakati mwingine wanaendesha baiskeli, lakini tulilazimika kuwazuia kwa sababu huwezi kujua nini kingetokea. Tulianza kuwapeleka shuleni na kuwarudisha nyumbani jioni,” alisema.

“Binti yangu alikuwa katika shule ya bweni na ilikuwa afueni kwamba asingefikiwa na mitandao ya kijamii. Lakini ilikuwa hali mbaya kwa watoto wangu wa kiume kusikia ‘baba yao ameua mtu’.”

Athari

Wanaomsimamia mwanariadha huyu walimtenganisha na mitandao ya kijamii kufuatia dhuluma hiyo, lakini alisema hakuwahi kufikiria kufuta akaunti zake.

“Lau ningefuta akaunti zangu katika mitandao ya kijamii, basi ingeonyesha kuwa kulikuwa na kitu ambacho ninaficha. Ningali na akaunti zangu. Sikufanya lolote,” alisema.

Hata hivyo, anaamini matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yaliathiri utendaji wake katika mashindano.

Kipchoge aliibuka wa 10 katika mbio za Tokyo Marathon mnamo Machi 3, 2024.

Yalikuwa matokeo ya chini zaidi tangu aanze mchezo wa riadha mwaka wa 2013, akitia nanga kwa dakika mbili na nusu nyuma ya mshindi Benson Kipruto.

“Nilipokuwa Tokyo sikulala kwa siku tatu,” alifichua.

“Hayo yalikuwa matokeo yangu mabaya zaidi kuwahi kutokea.”

Baada ya kukabiliwa na vitisho na unyanyasaji mitandaoni, Kipchoge anaamini kuwa kampuni za mitandao ya kijamii “hazijachukua hatua” kuzuia unyanyasaji kwenye majukwaa yao.

“Hawa watu ‘wasio na uso’ huchapisha mambo mabaya na ni hatari sana,” alisema.

“Ukishtaki baadhi ya akaunti kampuni husika huchukua muda kuzifunga akaunti hizo,” akaongezea.

Hata hivyo, Kipchoge amefurahia tangazo kutoka kwa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC).

IOC inapanga “kuchukua hatua kikamilifu” ili kuwalinda wanariadha dhidi ya unyanyasaji mtandaoni wakati wa Mashindano ya Olimpiki ya Paris 2024 nchini Ufaransa.

  • Tags

You can share this post!

Mungiki wadaiwa kutesa, kuibia abiria Karatina

Jinsi misako ya kushtukiza inavyonasa ‘mapedi’...

T L