Eliud Kipchoge, Timothy Cheruiyot waorodheshwa kuwania tuzo ya mwanariadha bora duniani
Na GEOFFREY ANENE
MWANARIADHA bora duniani wa mwaka 2018 Eliud Kipchoge yumo mbioni kushinda taji hili kwa mara ya pili mfululizo baada ya Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) kumjumuisha Ijumaa katika orodha ya wawaniaji 11.
Bingwa huyu wa Olimpiki anashikilia rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 42 duniani ya saa 2:01:39 kutoka Berlin Marathon mwaka 2018 na pia ni binadamu wa kwanza kukamilisha umbali huo chini ya saa mbili alipomaliza mbio maalum za INEOS 1:59 Challenge kwa saa 1:59:40 jijini Vienna nchini Austria mnamo Oktoba 12, 2019.
Mkimbiaji huyu mwenye umri wa miaka 34, ambaye alishinda London Marathon mwezi Aprili, anawania taji la mwanariadha bora duniani dhidi ya Mkenya mwenzake Timothy Cheruiyot, ambaye ni bingwa wa dunia wa mbio za mita 1,500 na pia Riadha za Dunia za Diamond League.
Wakenya hawa watakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa mabingwa wa dunia Donavan Brazier (mita 800), Christian Coleman (mita 100), Sam Kendricks (kuruka kwa fito), Noah Lyles (mita 200 na mita 4×100) na Christian Taylor (Triple Jump) kutoka Amerika.
Orodha hii inakamilishwa na bingwa wa mbio za nyika duniani na mita 10,000 Joshua Cheptegei (Uganda), raia wa Bahamas Steven Gardiner ambaye ni bingwa wa dunia wa mbio za mita 400 na hajashindwa katika kitengo hiki mwaka huu, mfalme wa kutupa tufe duniani Daniel Stahl (Uswidi) na raia wa Norway Karsten Warholm, ambaye amefagia kila taji ndani na nje ya uwanja la mbio za mita 400 kuruka viunzi mwaka huu.
Kura za kuchagua mmoja wa wanariadha hawa kuwa mwanariadha bora wa mwaka hapo Novemba 23 mjini Monaco, tayari zimeanza kupigwa.
Baraza la IAAF na familia ya IAAF zitatuma kura zao kupitia kwa baruapepe, huku mashabiki wakichangia kura zao kupitia kwa mitandao ya kijamii ya IAAF ya Facebook, Twitter na Instagram.
Baraza la IAAF linachangia asilimia 50 ya kura nazo familia kwa maana ya familia ya IAAF na mashabiki, wakichangia asilimia ya kura 25 kila mmoja.
Upigaji wa kura za kitengo hiki cha wanaume utafungwa Novemba 4.
Kufikia mwisho wa upigaji kura, wawaniaji watano ndio watasalia mbioni na kufahamu hatima yao katika hafla ya kupeana tuzo hiyo ya kifahari mnamo Novemba 23. Wawaniaji wa kitengo cha wanawake watatangazwa Oktoba 15.
Kipchoge ni Mkenya wa pili kutwaa taji hili baada ya mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za mita 800 David Rudisha mwaka 2010.
Hakuna mwanariadha mwanamke kutoka Kenya amewahi kuibuka mwanariadha bora wa mwaka duniani.