Emerging Stars kikaangoni kufukuzia tiketi ya Olimpiki
Na GEOFFREY ANENE
KENYA inakabiliwa na kibarua kigumu cha kufuta kichapo cha mabao 2-0 ilichopata dhidi ya Sudan katika mechi ya mkondo wa kwanza ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika kwa wachezaji wasiozidi umri wa miaka 23 zitakaporudiana leo Jumanne uwanjani Kasarani jijini Nairobi.
Vijana wa kocha Francis Kimanzi wanahitaji kulemea Sudan kwa mabao 3-0 ili kusalia katika vita hivi vinavyotumika pia kufuzu kushiriki michezo ya Olimpiki mwaka 2020.
Kenya haijawahi kushiriki soka katika Olimpiki tofauti na Sudan iliyokuwa katika makala ya mwaka 1972 nchini Ujerumani.
Timu ya Kenya maarufu Emerging Stars ilianza kampeni yake vyema pale ilipokung’uta Mauritius kwa jumla ya mabao 8-1 mwezi Novemba 2018 katika raundi ya kwanza.
James Mazembe, ambaye alipachika bao moja Stars ikilima Mauritius 5-0 katika mechi ya mkondo wa kwanza uwanjani Kasarani na tena ikishinda 3-1 nchini Mauritius, ni mmoja wa wachezaji Kenya itatumai ataamka vyema kuongoza uwindaji wa ushindi mkubwa.
Sudan ilipata ushindi mwembamba wa mabao 2-1 dhidi ya wanavisiwa wa Ushelisheli katika raundi hiyo.
Mchuano kati ya Kenya na Sudan utasimamiwa na refa Andofetra Rakotojaona akisaidiwa na raia wenzake kutoka Madagascar Velomanana Ferdinand na Randrianarivelo Ravonirina (wanyanyuaji vibendera) na Ben Amisy Tsimanohisty (afisa wa nne).
Lewis Blaze Madeleine kutoka Ushelisheli ameteuliwa kuwa kamishna wa mechi naye Louzaya Rene Daniel kutoka Congo ni mtathmini wa waamuzi.
Mshindi kati ya Kenya na Sudan ataingia raundi ya tatu kumenyana na ama Nigeria au Libya kutegemea ni timu gani itakuwa imezidi nyingine.
Raundi ya tatu itaamua washiriki wa Kombe la Afrika kwa wachezaji wasiozidi umri wa miaka 23, ambalo wanamedali wataingia Olimpiki mwaka 2020.
Kwingineko, timu ya Harambee Stars ilirejea nchini mapema jana kutoka Ghana ilikokamilisha mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) kwa kuchapwa 1-0 mjini Accra mnamo Machi 23.
Vijana wa kocha Sebastien Migne walikuwa tayari wamefuzu kutoka Kundi F pamoja na Ghana kabla ya mechi hiyo ya marudiano.
Nchi 24 ikiwemo Kenya inayorejea katika AFCON tangu mwaka 2004 zitakuwa nchini Misri mwezi Juni/Julai kuwania ubingwa. Droo itafanywa Aprili 12.