Michezo

Ephrem Guikan, kituko uwanjani na kero kwa mashabiki

January 17th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA CECIL ODONGO

MSHAMBULIZI wa Gor Mahia, Ephrem Guikan amewaomba radhi mashabiki wa miamba hao baada ya kuondoka uwanjani kwa hasira za mkizi wakati wa mechi ya KPL dhidi ya Mount Kenya United siku ya Jumatano Januari 16.

Raia huyo wa Uganda alipandwa na za kwao alipoondolewa uwanjani ili kumpisha nyota wa zamani wa Harambee Stars Dennis Oliech katika dakika ya 60, hatua ambayo haikumfurahisha kisha akaelekea moja kwa moja hadi chumba cha kubadilisha nguo badala ya kujiunga na benchi la kiufundi.

“Naja kwenu na ujumbe wa kuomba msamaha kutokana na tabia yangu isiyofaa wakati wa mechi dhidi ya Mount Kenya. Kwa kweli nilikasirika sana. Nawaomba radhi mashabiki wote, benchi la kiufundi na kocha. Najutia kitendo changu, mnisamehe,” akaandika mwanadimba huyo katika ukurasa wake wa Twitter.

Awali, mashabiki waliokerwa na tabia ya Guikan walisikika wakiapa kwamba hawatamruhusu tena kuvalia jezi ya timu yao na kumtaka aondeke mara moja iwapo anaona hathaminiwi tena na kocha.

“Huyu ni straika aina gani anatolewa uwanjani na badala ya kushukuru anafokafoka na kuelekea katika chumba cha wachezaji badala ya kujiunga na wenzake?. Hatutakubali Guikan aicheze Gor Mahia tena,” akasikika shabiki moja akisema baada ya mechi.

Hata hivyo, Oliech aliishia kudhihirisha kuingizwa kwake alipofunga bao safi dakika chache baadaye katika mechi ambayo mshambulizi wa K’Ogalo raia wa Uganda Erissa Ssekisambu alifunga mabao matatu na kusaidia timu kupata ushindi wa 4-1 dhidi ya wapinzani.

Mwanadimba huyo hata hivyo si geni katika mawanda ya kuzua sarakasi anapohisi anadhulumiwa au kuonewa wakati, baada au kabla ya mechi.

Jumatano Januari 9 wiki jana, Guikan alikasirika na kuzua drama alipogundua kwamba jina lake lilikosa katika orodha ya wachezaji 18 waliotajwa na K’Ogalo kushiriki mechi ya ligi dhidi ya Posta Rangers.

Guikana alifokafoka na kujizungumzia kama mwehu kisha akaondoka moja kwa moja mbele ya wenzake na kuelekea kituo cha mabasi kuabiri gari la kurejea mtaani. Imekuwa ikikisiwa kwamba uhusiano mbaya kati yake na kocha Hassan Oktay imekuwa ikichangia kulishwa kwake benchi.

Hata hivyo Afisa Mkuu Mtendaji wa Gor Mahia Omondi Aduda alijitokeza kumtetea na kukanusha kwamba Oktay na Guikan hawakuwa wakionana uso kwa macho.