Michezo

EPL: Klopp na Guardiola, nani mkali?

January 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA wa Liverpool, Jurgen Klopp ameipaka Manchester City mafuta kwa mgongo wa chupa kabla ya fataki kati yao uwanjani Etihad, Alhamisi.

Licha ya Liverpool kulemea City mara nane, kuchapwa mara moja na kutoka sare mechi tatu katika mechi 12 zilizopita katika mashindano yote, Mjerumani Klopp anasema mabingwa hawa watetezi wa Uingereza “ni timu bora duniani.”

Vijana wa Klopp watateremka uwanjani Etihad wakiongoza jedwali kwa alama 54 dhidi ya nambari tatu City, ambayo iko alama saba nyuma.

Mabingwa mara 18 Liverpool, ambao wanatafuta taji lao la kwanza tangu msimu 1989/90, hawajapoteza mechi ya ligi msimu huu tofauti na City wanaouguza vichapo kutoka kwa Chelsea, Crystal Palace na Leicester.

“Ni mechi ngumu sana, ngumu ambayo unaweza kusakata katika ulimwengu wa soka wakati huu,” Klopp aliambia wanahabari Jumatano.

“Lazima tujiandae vilivyo, tuwe na ujasiri, tuwe na hamasa, hasira…, lakini ufahamu wetu kuhusu mpinzani huyu, kivyangu, bado yeye ni timu bora duniani.”

Klopp na Guardiola wote wamezungumzia nguvu ya upinzani kabla ya mchuano huu wa 21, huku Mhispania Guardiola akiisifu Liverpool pia kuwa namba wani duniani.

Liverpool imedondosha alama sita pekee msimu huu na itaingia mchuano huu na motisha ya kuponda wapinzani tisa waliopita ligini.

“The Reds” wameshinda mechi tatu kati ya nne zilizopita dhidi ya City, ingawa ziara yao ya mwisho ya ligi uwanjani Etihad iliishia kuwa kilio cha mabao 5-0 Septemba mwaka 2017. Chipukizi Gabriel Jesus na Leroy Sane walifunga mabao mawili kila mmoja siku hiyo baada ya Sergio Aguero kuanzisha maangamizi hayo. Sadio Mane, Mohamed Salah na Roberto Firmino, ambao ni baadhi ya washambuliaji katili nchini Uingereza, walishiriki mechi hiyo, lakini hawakuwa na lao. Mane alilishwa kadi nyekundu katika kipindi cha kwanza.

Guardiola ametaja mechi hii kuwa ya kufa-kupona ya City akisema matumaini ya kuwania taji yatakwisha vijana wake wakiwachwa kwa alama 10.