EPL kurejelewa Juni 12 serikali Uingereza ikiidhinisha mapendekezo yaliyopo mezani
Na CHRIS ADUNGO
HUENDA Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ikarejelewa Juni 12, 2020 iwapo Serikali ya nchi hiyo itaidhinisha baadhi ya mapendekezo yaliyojadiliwa katika mkutano uliohusisha vinara wa klabu zote 20 za kipute hicho mnamo Ijumaa.
Mbali na mechi zote zilizosalia kusakatiwa ndani ya viwanja vitupu visivyo na mashabiki, hakuna kikosi kitakachocheza katika uwanja wake wa nyumbani.
Maafikiano ya mkutano wa Ijumaa yalikuwa vikosi vyote kuazimia haja ya kukamilisha kampeni za EPL msimu huu chini ya maagizo ya serikali kuhusu kanuni mpya za afya.
Awali, Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson, alikuwa ameashiria uwezekano wa kulegezwa kwa masharti ya kanuni hizo kwa vikosi vya EPL ila hatua hiyo ingechukuliwa tu baada ya Alhamisi ya wiki ijayo.
Klabu za EPL zinatarajia kuanza mazoezi kufikia Mei 18 kwa minajili ya kuanza upya kampeni za kivumbi hicho msimu huu mnamo Juni 12.
Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Uingereza, huenda mashabiki wakasalia kufungiwa nje ya viwanja hata msimu ujao kwa kuwa kipindi cha kuruhisiwa kwao kuanza kuhudhuria mechi za vikosi vyao bado hakijabainika.
Hata hivyo, ilikubaliwa kwamba mechi zote za msimu huu zitapigiwa katika viwanja mahsusi vitakavyoteuliwa katika maeneo mbalimbali nchini Uingereza.
Hatua hiyo inanyima vikosi vyote nafuu ya kusakatia baadhi ya mechi katika nyuga zao za nyumbani.
Uteuzi wa viwanja vitakavyotumiwa kufanikisha taratibu zote za kurejelewa kwa michuano ya EPL utafanywa na maafisa wa usalama watakaoshirikiana na kitengo husika cha Idara ya Polisi nchini Uingereza.
Uwanja wa London unaomilikiwa na West Ham United, Emirates wa Arsenal na Etihad wa Manchester City ni miongoni mwa viwanja ambavyo tayari vimependekezwa na washikadau.
Viwanja vingine vinavyotarajiwa kuidhinishwa baada ya maafisa wa usalama kutathmini usalama wao ni Amex (Brighton), St Mary’s (Southampton), King Power (Leicester City), Villa Park (Aston Villa), Old Trafford (Man-United) na uwanja wa kitaifa wa Wembley jijini London.
Vinara wote wa klabu 20 za EPL wanatarajiwa kukutana tena mnamo Jumatatu ya Mei 18, 2020. Mkutano huo ulikuwa hapo awali umeratibiwa kufanyika Mei 15.