Erick ‘Marcelo’ Otieno apata dili tamu klabuni Rakow Czestochowa
Na GEOFFREY ANENE
BEKI wa kupanda na kushuka wa pembeni kushoto Erick ‘Marcelo’ Otieno amejiunga na klabu ya Rakow Czestochowa kutoka AIK nchini Uswidi kwa kandarasi ya miaka mitatu baada ya kupita vipimo vya afya.
Kandarasi yake na mabingwa hao wa Poland itakatika Desemba 31, 2026, ingawa amepewa fursa ya kuiongeza kwa miaka miwili.
Katika kandarasi na waajiri wake wapya, Marcelo, ambaye pia alimezewa mate na Espanyol nchini Uhispania, anatarajiwa kupata mshahara unaozidi Sh919,609.25 (PLN 23,000) aliopata kila wiki akiwa AIK. Kandarasi yake ya AIK iliratibiwa kufika tamati Desemba 2024.
Kuna tetesi kuwa atakula mshahara wa Sh1.6 milioni kwa wiki. Kwa sasa, mchezaji anayepokea mshahara mkubwa kambini mwa Rakow ni Mjerumani Sonny Kittel (Sh1.3m).
Ripoti zinasema AIK itapata mapato ya kati ya Sh23.9 milioni (PLN 600,000) na Sh31.9m (PLN 800,000) kwa kuuza Otieno.
Marcelo, ambaye alizaliwa Septemba 27, 1996, amekuwa Uswidi tangu mwaka 2018.
Alianzia soka yake ya watu wazima katika klabu ya Gor Mahia FC mnamo Januari 1, 2016.
Marcelo alihama Gor mnamo Januari 18, 2017, na kuelekea Kolkheti-1913 mnamo Januari 1, 2018 baada ya kuchezea klabu hiyo ya Georgia mara 20.
Kisha, Marcelo alinyakuliwa na KS Kastrioti nchini Albania kabla ya kuingia Uswidi mnamo Julai 1, 2018 kuchezea Vasalunds IF nchini Uswidi inayoshirikiana na AIK.
Mchezo wake mzuri Vasalunds ulivutia AIK kumsaini Januari 1, 2020. Ameondoka AIK akiwa ameichezea mara 104, kuifungia mabao manne na kuchngia pasi za mwisho 15 zilizozaa magoli.
Marcelo, ambaye amewaacha Wakenya Collins Sichenje na Henry Meja kambini mwa AIK, amechezea timu ya taifa ya Harambee Stars mara 38.
Ameshukuru familia ya AIK, wachezaji wenza, makocha, wasimamizi na mashabiki kwa kumuunga mkono akiwa kambini mwa klabu hiyo.
“Tulipata kumbukumbu nzuri pamoja na nitashukuru daima kuwa nilipata kuvalia jezi ya AIK mara 104,” akasema mwanafunzi huyo wa zamani wa Kakamega School.
Rakow ilithibitisha kupata huduma za Mkenya huyo ikimsifu kwa kuwa stadi katika nafasi anayocheza kwa miaka kadhaa nchini Uswidi.
“Erick ni mchezaji anayeafiki filosofia yetu kabisa. Ana kasi, anajituma vilivyo na anacheza kwa bidii. Sifa zake akiwa na mpira na uwezo wa kutumia miguu yake yote zitatusaidia katika pembe zote kama mchezaji atakayetumiwa katika mfumo wetu,” mkurugenzi wa michezo wa Rakow, Samuel Cardenas, amesema.
Ameongeza, “Tunasubiri kuona Erick akivalia jezi yetu kwa sababu anatamani sana kupigania mataji zaidi na kuthibitisha kazi yake katika mashindano ya Ulaya.”
Rakow kwa sasa inakamata nafasi ya nne kati ya washiriki 18 kwenye Ligi Kuu ya Poland ambayo imefika katikati.