Eriksen pua na mdomo kuyoyomea Real
Na MASHIRIKA
LONDON, UINGEREZA
KOCHA Mauricio Pochettino wa Tottenham Hotspur amesema kwamba hana uhakika iwapo mchuano wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) uliowakutanisha na Newcastle United mwishoni mwa wiki jana ulikuwa wa mwisho kwa mfumaji Christian Eriksen kuchezea kikosi hicho.
Eriksen ambaye ni mzawa wa Denmark amekuwa akihusishwa na uwezekano mkubwa wa kuingia katika sajili rasmi ya Real Madrid kufikia Septemba 2 ambapo muhula wa uhamisho wa wachezaji wa Ligi Kuu ya Uhispania unatarajiwa kutamatika.
Mkataba kati ya Eriksen na Tottenham unatarajiwa kutamatika rasmi mwishoni mwa msimu ujao. Sogora huyo mwenye umri wa miaka 27 aliwajibishwa na kikosi hicho katika kipindi cha pili mwishoni mwa wiki jana ambapo walipokezwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa wageni wao Newcastle.
“Tunasubiri kuona kitakachofanyika. Hali ya sasa inayomkabili Eriksen ni ngumu kwa kuwa anafahamu kwamba maamuzi atakayoyafanya yakuwa na athari ya moja kwa kikosi kizima,” akasema Pochettino.
Licha ya kujivunia asilimia 80 ya umiliki wa mpira dhidi ya Newcastle, Spurs walikosa ubunifu kila walipopata mpira katika safu ya kati.
Isitoshe, washambuliaji wao walisalia butu katika vipindi vyote vya mchezo huku wakilenga shabaha kwenye lango la wapinzani mara mbili pekee.
“Unapopoteza mechi, masogora ambao hawakucheza huchukuliwa kuwa ndio bora. Kocha hukosolewa pakubwa kutokana na uteuzi wake wa kikosi cha kwanza. Maswali yasingekuwapo kabisa iwapo Spurs wangesajili ushindi wa 3-0 dhidi ya Newcastle,” akasema Pochettino.
Kuaga bila ada
Ilivyo, huenda Eriksen akaagana na Spurs bila ada yoyote msimu ujao iwapo atakataa kurefusha muda wa kuhudumu kwake kambini mwa waajiri wake wa sasa.
Katika kile ambacho kimefasiriwa kuwa jitihada za Spurs kujiandaa kwa maisha bila ya Eriksen, Pochettino aliwashawishi waajiri wake mwishoni mwa msimu jana kufungulia mifereji ya pesa na kujinasia huduma za wanasoka stadi.
Miongoni mwa wachezaji walioingia katika sajili rasmi ya Tottenham ni Tanguy Ndombele aliyeagana na Olympique Lyon ya Ufaransa kwa kima cha Sh7 bilioni na kiungo Giovani Lo Celso aliyetokea Real Betis kwa mkopo wa mwaka mmoja.