Michezo

Essien ateuliwa kocha msaidizi katika klabu ya Nordsjaelland nchini Denmark

September 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

NGULI wa soka kutoka Ghana, Michael Essien, 37, ameteuliwa kuwa kocha msaidizi wa kikosi cha FC Nordsjaelland nchini Denmark.

Kiungo huyo wa zamani wa Chelsea atasalia pia kuwa mchezaji wa kikosi hicho huku akijiendeleza kitaaluma kwa kusomea ukocha katika kiwango cha UEFA A kupitia Shirikisho la Soka la Uingereza (FA).

Kikosi cha Nordsjaelland kinamilikiwa na kampuni ya Right to Dream iliyo na makao makuu nchini Ghana.

Essien atakuwa chini ya uelekezi wa kocha Flemming Pedersen ambaye kwa sasa anadhibiti mikoba ya Nordsjaelland.

“Nina furaha kubwa ya kujiunga na benchi ya kiufundi ya kikosi hiki ambacho pia kimenipa jukwaa la kujiendeleza kitaaluma,” akasema Essien kwa kusisitiza kwamba atakuwa mchezaji kwa wakati mwingine na kocha pia.

Mbali na Chelsea, Essien aliwahi pia kuvalia jezi za Real Madrid nchini Uhispania na Olympique Lyon inayoshiriki Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1).