Michezo

Ethiopia yainyang'anya Kenya ubingwa mita 3,000

July 16th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

BAADA ya kushinda medali ya dhahabu katika makala 15 mfululizo katika mbio za wanaume za mita 3,000 kuruka viunzi na maji kwenye Riadha za Dunia za Under-20, Kenya ilisalimu amri mjini Tampere nchini Finland, Julai 15, 2018.

Mwakilishi wa pekee wa Kenya katika fainali ya makala ya 17, Leonard Bett, aliridhika katika nafasi ya pili, huku Ethiopia ikivunja tamaduni hiyo ya Kenya kupitia Takele Nigate.

Kenya ilikuwa imeshinda kitengo hiki kupitia William Koskei (1988), Matthew Birir (1990), Jimmy Muindi (1992), Paul Chemase (1994), Julius Chelule (1996), Reuben Kosgei (1998), Raymond Yator (2000), Mike Kipyego (2002), Ronald Rutto (2004), Willy Komen (2006)Jonathan Ndiku (2008 na 2010), Conseslus Kipruto (2012), Barnabas Kipyego (2014) na Amos Kirui (2016) kabla ya kupigwa breki.

Licha ya kupoteza taji la mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji za wanaume, Kenya ilifaulu kurejesha ubingwa wa dunia ambao ulikuwa umeiponyoka katika makala matatu yaliyopita.

Ilimaliza katika nafasi ya kwanza katika mashindano ya mwaka 2018 yaliyoshirikisha mataifa 158.

Msimamo wa medali (10-bora):

Timu   Dhahabu   Fedha        Shaba        Jumla

Kenya        6       4       1       11

Jamaica     4       5       3       12

Marekani   3       7       7       17

Ethiopia     3       2       4       9

Uingereza  3       1       2       6

A.Kusini     3       0       1       4

Australia    2       3       0       5

Japan        2       2       2       6

Ujerumani  2       0       2       4

Mexico       2       0       0       2