Michezo

Euro 2024: Wenyeji Ujerumani, kuanzisha ngoma Ijumaa usiku dhidi ya Scotland

June 14th, 2024 2 min read

MUNICH, Ujerumani

Wenyeji Ujerumani wanatarajiwa kuanza Kombe la Ulaya (Euro 2024) kwa kishindo watakapomenyana na Scotland katika mechi ya Kundi A ugani Allianz Arena Ijumaa, Juni 14, 2024 usiku.

Wajerumani, ambao walishinda makala ya 1972, 1980 na 1996, wana rekodi nzuri dhidi ya Scotland.

Vijana wa kocha Julian Nagelsmann wamepiga Scotland mara sita na kutoka sare mara mbili katika mechi nane wamekutana mashindanoni na kupoteza mchuano mmoja wa kirafiki.

Mechi ya leo inatarajiwa kushuhudia mabao mengi.

Ujerumani almaarufu Die Mannschaft walicheza mechi yao ya mwisho ya kujipima nguvu dhidi ya Ugiriki ugani Borussia-Park hapo Juni 7.

Wajerumani walilemea Wagiriki 2-1 kupitia mabao ya Kai Havertz anayechezea klabu ya Arsenal na Pascal Gross wa Brighton & Hove Albion.

Scotland nao walialika Finland katika mechi ya mwisho ambayo iliishia kuwa sare ya 2-2. Lawrence Shankland alifunga Scotland magoli yote mawili.

Katika mechi zao 10 zilizopita, Ujerumani wamezoa ushindi mara tatu, kupoteza mara mbili na kutoka sare mara tano.

Havertz na Ilkay Gundogan wanaongoza ufungaji wa mabao ya Ujerumani wakiwa na matano kila mmoja naye Jonas Hofmann ana matatu. Serge Gnabry ndio anaongoza kusuka asisti nyingi baada ya kuchangia nne.

Kiungo mshambulizi Florian Wirtz alikuwa na msimu mzuri 2023-2024 na Bayer Leverkusen kwa hivyo ni mmoja wa wachezaji Ujerumani itategemea kwenye mashindano hayo ya taifa 24.

Katika mechi zao 10 zilizopita, Scotland ya kocha Steve Clarke wametawala sita, kupoteza moja na kutoka sare mara tatu. Licha ya kuwa na rekodi mbaya dhidi ya Ujerumani, inamaanisha kuwa Scotland pia si wachache.

Mshambulizi wa Manchester United, Scott McTominay ndiye mkali zaidi kambini mwa Scotland. Ana mabao saba akifuatiwa na John McGinn (matatu) na Stuart Armstrong (moja).

Andrew Robertson ni mmegaji wa asisti nyingi akiwa na tatu.

Kufuzu tu kushiriki Euro 2024, kila timu ilipata Sh1.2 bilioni. Ukishinda mechi ya makundi, unaongezwa Sh139.1 milioni nayo sare unapata Sh69.5m.

Ukiingia 16-bora, utaongezwa Sh208.6m na robo-fainali Sh347.7m. Timu zitakazofika nusu-fainali zitaongezwa Sh556.4 milioni. Mabingwa na nambari mbili wataongezwa Sh1.1 bilioni na Sh695.4 milioni, mtawalia.

Vikosi vitarajiwa:

Ujerumani; Neuer; Kimmich, Tah, Rudiger, Mittelstadt; Kroos, Andrich; Musiala, Gundogan, Wirtz; Havertz.
Scotland; – Gunn; Hendry, Hanley, Tierney; Ralston, McTominay, Gilmour, Robertson; McGinn, Christie; Shankland.

Ratiba:

Juni 14 – Ujerumani vs Scotland (Kundi A, 10.00pm); Juni 15 – Hungary vs Uswisi (Kundi A, 4.00pm), Uhispania vs Croatia (Kundi B, 7.00pm), Italia vs Albania (Kundi B, 10.00pm); Juni 16 – Poland vs Uholanzi (Kundi D, 4.00pm), Slovenia vs Denmark (Kundi C, 7.00pm), Serbia vs Uingereza (Kundi C, 10.00pm).