Michezo

Euronuts kutetea ubingwa Chapa Dimba Mkoa wa Kati

April 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya wavulana ya Euronuts ya Kiambu ambayo ndiyo bingwa mtetezi katika Mkoa wa Kati kwenye mechi za Chapa Dimba na Safaricom Season Two, ilijikatia tiketi ya fainali ilipozoa bao 1-0 dhidi ya Irigiro Boys kutoka Maragua kwenye nusu fainali iliyochezewa Thika Stadium mjini humo.

Nayo Lufa Graduates ya Laikipia ilibeba ufanisi wa mabao 2-0 mbele ya Tetu Boys ya Nyeri na kufuzu kwa fainali.

Kitengo cha wasichana, bingwa mtetezi Limuru Starlets na Barcelona Ladies ziliangusha JYSA na Kirinyaga Dynamo kwa bao 1-0 na 4-1 mtawalia na kufuzu kwa fainali msimu huu.

”Tuna fuaraha tele tulishusha mechi safi dhidi ya wapinzani wetu na kufaulu kujikatia tiketi ya fainali pia nilifaulu kufunga magoli manne ndani ya mchezo mmoja,” mchezaji wa Barcelona Ladies, Jane Njeri alisema na kuongeza kuwa huenda akatwaa tuzo ya mfungaji bora.

JANE Njeri (kulia) wa Barcelona Ladies akishindana na Bancy Ngonyo wa Kirinyaga Dynamo kwenye nusu fainali ya wasichana kupigania ubingwa wa Mkoa wa Kati katika pambano la Chapa Dimba na Safaricom Season Two Uwanjani Thika Stadium, Thika. Barcelona Ladies ilishindwa kwa mabao 2-0. Picha/ John Kimwere

Nayo Limuru Starlets ilifanya kweli kupitia Nakag Swan huku Eliza Mithamo akitingia Kirinyaga Dynamo. Kwenye mechi za wavulana Lufa Graduates ilizoa ushindi kupitia mabao ya Johnson Gikonyo na Fredrick Maraka waliotikisa wavu mara moja kila mmoja.

Naye Mengitsu Lual aliifungia Euronuts bao la pekee kwenye patashika iliyoshuhudia ushindani wa kufa mtu.

”Msimu huu tunataka ubingwa wa Mkoa na kufuzu kushiriki fainali za kitaifa maana tumejiandaa kukabili upinzani wowote utakaofika mbele yetu,” kocha Joseph Jagero wa Lufa Graduates alisema.

Timu itakayobeba ubingwa wa Mkoa huo kwa wavulana na wasichana kila moja itatia mfukoni kitita cha Sh200,000 kando na tiketi ya kufuzu kushiriki fainali za kitaifa msimu huu. Fainali za msimu huu zitaandaliwa mwezi Juni mwaka huu katika uwanja wa Kinoru Stadium, mjini Meru.