Michezo

Euronuts wasema Sh1 milioni za Chapa Dimba ni zao

April 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

CHIPUKIZI wa Euronuts FC kutoka Kiambu wamedai kwamba wamekaa vizuri kutesa wapinzani wao na kutawazwa wafalme wa kitaifa katika pambano la Chapa Dimba na Safaricom Season Two mwaka huu.

Kocha wake, Solomon Muoni amedokeza kuwa wachezaji wake kamwe hawana cha kuhofia ingawa wapo wachezaji wachache wanaouguza majeraha.

”Natumai watakuwa hali nzuri kabla ya kinyang’anyiro hicho,” alisema na kuongeza kuwa wachezaji 12 wamekuwapo pamoja tangia mwaka uliyopita. Euronuts mabingwa wa Mkoa wa kati kwenye ngarambe hiyo itakuwa ikishiriki fainali za kitaifa kwa mara ya pili baada ya kushiriki msimu uliyopita.

Kocha huyo ameapa kwamba ana imani wachezaji wake watafitua vumbi la kufa mtu kwenye michuano hiyo. “Hakika itakuwa vigumu kwa timu yoyote kushinda chipukizi wangu endapo itateleza na kushindwa kuwafunga ndani ya kipindi cha kwanza,” alisema.

Akizungumza na Taifa Dijitali kocha huyo alisema kiasi anahofia timu ya Manyatta Boys kutoka Mkoa wa Nyanza lakini baada ya dakika tisini dimbani watakuwa pazuri kufahamu mbichi na mbivu.

Chipukizi hao chini ya nahodha, Steven Duol walinasa tiketi ya kufuzu kwa fainali hizo walipotandika Lufa Graduates kwa mabao 2-1 katika fainali iliyochezewa Thika Stadium, mjini humo.

VINCENT Nyamote (kushoto ) wa Tetu Boys akijaribu kumkwepa mpinzani wake, Fredrick Maraca wa Lufa Graduates kwenye nusu fainali ya wavulana kuwania ubingwa wa Mkoa wa Kati katika pambano la Chapa Dimba na Safaricom Season Two Uwanjani Thika Stadium, Thika. Picha/ John Kimwere

Katika nusu fainali, Euronuts iliiranda Irigio Boys kutoka Maragua kwa bao 1-0 nayo Lufa Graduates ya Laikipia ilivuna ufanisi wa mabao 2-0 mbele ya Tetu Boys ya Nyeri.

Ili kutinga fainali za Mkoa huo, Euronuts ilifanya kazi kubwa kwenye mechi za mashinani ilipofanikiwa kushiriki jumla ya mechi nane, kushinda michezo minne kisha kutoka nguvu sawa mara nne.

”Kwa misimu miwili sasa nimegundua kwamba mechi za kipute hicho za mashinani huhitaji ushindi na pengine kuteleza iwe kutoka nguvu sawa lakini kupoteza mchezo mmoja huwa njiani kubanduliwa,” kocha huyo alisema.

Euronuts inajivunia kukuza wachana nyavu wawili ambao huchezea klabu zinazoshiriki kandanda ya ligi za hadhi ya juu nchini. Imenoa kucha za John Njuguna na Ezekiel Nyakti wachezaji wa Ulinzi FC na Posta Rangers mtawalia.

Euronuts inajumuisha wachezaji kama: David Wainaina na Boniface Nyamora (walinda langa). Francis Kuna, Charles Gichuki, Anthony Njenga, George Ndungu na Robert Kinuthia (beki).

Safu ya kati wapo:George Mungai, Philip Ewoi, Eric Mirangi, Kelvin Mwaura na Jack Johnson. Washambulizi: Lual Mengistu, Steve Waiyaki, Bruno Steve na Allan Ogoye.

Meneja wake, Ronald Gathuri anawarai mashabiki wao kutowaacha ila anastahili kuandamana nao kuwapigia debe katika fainali hizo za mwezi Juni uwanjani Kinoru Stadium, Kaunti ya Meru. ”Sina budi kuipongeza Safaricom inafanya jambo nzuri linalochangia baadhi ya wachezaji chipukizi kutambua talanta zao,” meneja huyo alisema.

Aidha anashukuri kila mmoja aliyewahi kuwapiga jeki kwa vyovyote ikiwamo kuwashabikia kwenye juhudi za kushiriki mchezo huo tangu kikosi kianzishwe.

Timu zingine ambazo zimefuzu kwa fainali za mwaka huu ni: Super Solico Boys-wavulana na St Marys Ndovea-wasichana (Mashariki) Al Ahly na Kitale Queens wavulana na wasichana(Rift Valley), Lugari Blue Saints (wavulana) na Bishop Njenga Girls (Magharibi), Manyatta Boys na Ndhiwa Queens(Nyanza), Shimanzi Youth-wavulana na Changamwe Ladies(Mombasa) bila kusahau Euronuts Boys na Barcelona Ladies (Mkoa wa Kati).

Mabingwa wa kitaifa timu ya wavulana pia wasichana kila moja itatuzwa kitita cha Sh 1 milioni.