EUROPA HIYOO… Arsenal kukwaana na Eintracht Frankfurt
Na MASHIRIKA
FRANKFURT, Ujerumani
ARSENAL wataanza kampeni yao ya Europa League kwa ziara nchini Ujerumani ambapo watakutana na Eintracht Frankfurt leo Alhamisi usiku.
Ni mechi ambayo watahitaji ushindi baada ya kulazimishiwa sare ya 2-2 Jumapili katika mechi ya EPL ambayo waliongoza 2-0 katika kipindi cha kwanza kabla ya Watford kutoka nyuma na kusawazisha.
Kocha Unai Emery anatarajiwa kupanga kikosi chake kwa makini baada ya timu hiyo kuchanganyikiwa katika kipindi cha pili dhidi ya Watford kwenye mechi iliyochezwa Vicarage Road.
Jumapili, Arsenal ilionekana kurudia makosa ya awali ya kushindwa kuzuia wapinzani kufunga langoni mwao.
Mbali na makosa yao ya kawaida katika safu ya ulinzi, kadhalika vijana hao wa Unai walipoteza nafasi nyingi za kufunga.
Walipocheza mechi ya mwisho ya Europa League, Arsenal walicharazwa 4-1 na Chelsea jijini Boku katika fainali ya kuwania ubingwa huo.
Katika mechi ya leo, Franfurt watakuwa chini ya kocha mpya, Adi Hutter, akinoa kikosi ambacho kilitoka nyuma na kuibwaga Befica 4-2 na kufuzu kwa nusu-fainali ambapo kilipoteza kwa Chelsea.
Lakini kwa sasa, klabu hiyo ya Bundesliga inashikilia nafasi ya tisa jedwalini baada ya kupoteza nyota wawili, Luka Jovic aliyejiunga na Real Madrid na Senastian Haller aliyeyoyomea West Ham United. Mastaa hao kwa jumla waliifungia Frankfurt mabao 47, msimu uliopita.
Huku wakitarajia mashabiki wao kumiminika uwanjani kuwashangilia, Frankfurt wanatarajiwa kuzua upinzani mkali dhidi ya Arsenal.
Hata hivyo, wenyeji watakuwa bila Mijat Gacinovic aliyeumia mazoezini, pamoja na mshambuliaji Jonathan de Guzman anayetatizwa na jeraha la msuli.
Beki auguza jeraha
Beki wa kutegemewa, Marco Russ anauguza jeraha wakati hali ya Sebastian Rode na Goncalo Paciencia ikisubiriwa kabla ya uamuzi wa kikosi cha mwisho kufanywa.
Kwa upande wa Arsenal, mshambuliaji Alexandre Lacazette yuko nje hadi Oktoba kutokana na jeraha la kisigino, wakati Kieran Tierney akiendelea kufanya mazoezi mepesi baada ya kufanyiwa upasuaji mwaka uliopita.
Hector Bellerin, Rob Holding na Konstantinos Mavropanos wanaendelea kuuguza majeraha ya muda mrefu, ingawa wanatarajiwa kurejea mwezi ujao.
Vikosi, Eintracht Frankfurt: Trapp; Abraham, Hinteregger, Hasebe; Rode; Gregoritsch, Sow, Chandler, da Costa; Silva na Cordova.
Arsenal: Leno; Kolasinac, Luiz, Mustafi, Maitland-Niles; Xhaka, Willock, Torreira, Ozil; Aubameyang na Pepe.