Everton waangusha Tottenham kwa mara ya kwanza tangu 2012
Na MASHIRIKA
BAO la Dominic Calvert-Lewin katika kipindi cha pili lilitosha Everton kuwapiga Tottenham Hotspur 1-0 na kuwapa mwanzo bora katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu.
Calvert-Lewin alimwacha hoi kipa Hugo Lloris baada ya kuwazidi maarifa mabeki Toby Alderweireld na Eric Dier katika dakika ya 55. Goli hilo lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati ya Calvert-Lewin na Lucas Digne.
Ilikuwa mara ya kwanza kwa Everton kuwapiga Tottenham katika kivumbi cha EPL tangu 2012.
Ingawa Tottenham walianza mechi hiyo kwa matao ya juu, kipa Jordan Pickford alifanya kazi ya ziada kumnyima Dele Alli na Matt Doherty fursa maridhawa za kufunga mabao katika dakika za mapema.
Hata hivyo, ushawishi wa sajili mpya James Rodriguez aliyeagana na Real Madrid ulihisika pakubwa ugani na Everton wakaonekana kuwazidi nguvu wenyeji wao katika takriban kila idara.
Nusura Everton wajipate kifua mbele kupitia kwa Richarlson Andrade, lakini juhudi za Mbrazil huyo zikavurugwa na Lloris.
Chini ya kocha Ancelotti aliyetua ugani Goodison Park msimu uliopita, Everton walikamilisha kampeni za EPL katika nafasi ya 12, hii ikiwa nambari yao mbovu zaidi tangu 2003-04.
Hata hivyo, kikosi hicho kwa sasa kina kila sababu ya kutamba baada ya kusukwa upya hasa katika safu ya kati.
Mbali na Rodriguez, Everton wamemsajili pia Allan Loureiro kutoka Brazil na Abdoulaye Doucoure aliyeagana na Watford.
Rodriguez alichangia krosi tano za hakika, hii ikiwa idadi kubwa zaidi ya krosi kwa mchezaji katika mchuano wake wa kwanza wa EPL tangu Alexis Sanchez afanye hivyo kambini mwa Arsenal mnamo 2014.
Ilikuwa mara ya kwanza kwa kocha Jose Mourinho wa Tottenham kupoteza mechi katika siku ya kwanza ya msimu katika historia yake ya ukufunzi.
Tottenham kwa sasa wanajiandaa kuelekea Bulgaria kuvaana na Lokomotiv Plovdiv katika mchuano wa kufuzu kwa Europa League mnamo Alhamisi ya Septemba 17 huku Everton wakipepetana na Salford City mnamo Septemba 16 katika raundi ya pili ya Carabao Cup.
TAFSIRI: CHRIS ADUNGO