• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Everton wakomoa Crystal Palace na kudhibiti kilele cha jedwali la EPL

Everton wakomoa Crystal Palace na kudhibiti kilele cha jedwali la EPL

Na MASHIRIKA

DOMINIC Calvert-Lewin anaamini kwamba “nyakati bora zaidi” zaja katika taaluma yake ya usogora.

Hii ni baada ya kuongoza Everton kuwakomoa Crystal Palace 2-1 ugani Selhurst Park na kusaidia kikosi hicho kuendeleza mwanzo bora katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu wa 2020-21.

Calvert-Lewin, 23, kwa sasa anajivunia mabao matano kutokana na mechi tatu za mwanzo wa msimu huu. Ushirikiano mkubwa kati yake na Seamus Coleman na sajili mpya James Rodriguez unatarajiwa kuwatambisha Everton pakubwa katika kampeni za muhula huu chini ya mkufunzi Carlo Ancelotti.

Mwingereza huyo aliwafungulia Everton ukurasa wa mabao kunako dakika ya 10 kabla ya beki wa Senegal, Cheikhou Kouyate kusawazisha mambo katika dakika ya 26.

Richarlison Andrade alizamisha kabisa chombo cha wenyeji wao katika dakika ya 40 kupitia penalti iliyochangiwa na tukio la Joel Ward kuunawa mpira uliopigwa na Lucas Digne.

“Japo hatukucheza kwa ari zaidi jinsi tulivyofanya katika mechi mbili za kwanza msimu huu, tulijitahidi na kutia kapuni alama tatu muhimu. Natumai tutaendeleza ubabe huu katika nyingi za mechi zilizopo mbele na kuimarika hata zaidi hatua kwa hatua chini ya uongozi wa kocha wetu,” akasema.

Calvert-Lewin alifunga bao katika ushindi wa 1-0 uliosajiliwa na Everton dhidi ya Tottenham Hotspur katika mechi ya kwanza ya EPL msimu huu mnamo Septemba 13, 2020, kabla ya kupachika wavuni matatu katika ushindi wa 5-2 dhidi ya West Bromwich Albion mnamo Septemba 19 ugani Goodison Park.

Everton walishambulia sana wapinzani wao katika mechi hiyo huku Calvert-Lewin na Rodriguez wakimweka beki wa Palace, Mamadou Sakho katika ulazima wa kufanya kazi ya ziada.

Ingawa Palace walijitahidi pia kubisha lango la Everton mwishoni mwa kipindi cha pili, kipa Jordan Pickford alisalia tisti langoni na akapangua makombora mawili mazito ya Wilfried Zaha.

Ushindi wa Everton uliwadumisha kileleni mwa jedwali la EPL kwa alama tisa. Hii ni mara ya kwanza kwa Everton kusajili ushindi katika mechi tano mfululizo za mwanzo wa msimu mpya tangu 1938.

Aidha, ni mara ya kwanza kwa kikosi hicho kusajili ushindi kwenye mechi tatu mfululizo za EPL mwanzoni mwa msimu tangu 1993-94.

Palace kwa sasa watakuwa wageni wa Chelsea katika mchuano wao ujao wa EPL mnamo Oktoba 3, 2020 ugani Stamford Bridge huku Everton wakiwaalika West Ham United kwenye raundi ya nne ya Carabao Cup mnamo Septemba 30 kabla ya kuwa wenyeji wa Brighton ugani Goodison Park mnamo Oktoba 3, 2020.

  • Tags

You can share this post!

Wanne wakamatwa kwa kulaghai raia wa kigeni Sh29 milioni...

Chelsea watoka sare ya 3-3 dhidi ya West Bromwich Albion