Michezo

Everton yasajili James Rodriguez kutoka Real Madrid

September 8th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

EVERTON wamemsajili kiungo mvamizi raia wa Colombia, James Rodriguez kutoka kwa miamba wa soka ya Uhispania, Real Madrid.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 29 anaingia katika sajili rasmi ya Everton kwa mkataba wa miaka miwili. Uhamisho wa Rodriguez ambaye pia amewahi kuchezea Bayern Munich kwa mkopo wa miaka miwili, ulirasimishwa kwa kima cha Sh1.6 bilioni.

Rodriguez alijiunga na Real kutoka AS Monaco ya Ufaransa mnamo 2014 baada ya kuibuka mfungaji bora katika fainali za Kombe la Dunia zilizoandaliwa nchini Brazil mwaka huo.

Katika kampeni za msimu wa 2019-20, Rodriguez ambaye alikuwa na mwaka mmoja zaidi kwenye kandarasi yake na Real, aliwajibishwa na kocha Zinedine Zidane mara 14 pekee.

Hii ni mara ya tatu kwa Rodriguez kusajiliwa na kocha Carlo Ancelotti aliyewahi pia kumsajili wakati akidhibiti mikoba ya kikosi cha Real na Bayern Munich ya Ujerumani.

Anakuwa mchezaji wa tatu kusajiliwa na Everton ambao tayari wamejinasia huduma za kiungo matata mzawa wa Brazil, Allan kutoka Napoli na nyota wa timu ya taifa ya Ufaransa na klabu ya Watford, Abdoulaye Doucoure.

Rodriguez ambaye pia amewahi kuchezea FC Porto ya Ureno, anatazamiwa kufufu makali yak echini ya Ancelotti aliyepokezwa mikoba ya Everton mnamo Disemba 2019.

Akiwa kambini mwa Real, Rodriguez aliwanyanyulia miamba hao mataji mawili ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kabla ya kuyoyomea Bayern alikotwaa pia mataji mawili ya Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga).

Akivalia jezi za Porto, Rodriguez alisaidia miamba hao wa Ureno kutia kapuni mataji matatu ya Ligi Kuu na ushawishi wake ugani ukawa kiini cha Monaco kuweka mezani kima cha Sh5.3 bilioni kwa minajili ya huduma zake mnamo 2012.

Alifungia Monaco mabao 10 na kuchangia mengine 38 katika kipindi cha misimu mitatu. Rodriguez alipachika wavuni magoli sita katika fainali za Kombe la Dunia za 2014 zilizoshuhudia Ujerumani wakitawazwa mabingwa nchini Brazil.