• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:50 AM
FAHARI TELE: Wakenya watwaa dhahabu katika riadha michezo ya Afrika

FAHARI TELE: Wakenya watwaa dhahabu katika riadha michezo ya Afrika

Na CHRIS ADUNGO

WANARIADHA Benjamin Kigen na Lilian Kasait walitawala mbio za mita 3,000 kuruka maji na viunzi na mita 5,000 mtawalia kisha kuvunia Kenya nishani mbili za kwanza za dhahabu mnamo Jumatatu usiku katika Michezo ya bara la Afrika (AAG) inayoendelea jijini Rabat, Morocco.

Bingwa wa Olimpiki na Dunia katika mbio za mita 3,000 kuruka maji na viunzi, Conseslus Kipruto alijiondoa kivumbini zikisalia mizunguko miwili.

Mkenya mwingine Rop Joash Kiplimo alishindwa kukamilisha kinyang’anyiro hicho baada ya kujikwaa na kuanguka wakati wa mzungumko wa pili.

Kigen alifika utepeni baada ya muda wa dakika 8:12.39 mbele ya Wale Bayabl Getnet wa Ethiopia na Soufiane El Bakkali wa Morocco walioandikisha muda wa dakika 8:14.6 na 8:19.45 mtawalia.

Takele Malese na Bayabl wa Ethiopia waliongoza sehemu kubwa ya mbio hizo huku wakifuatwa unyo kwa unyo na Kipruto na El Bakkali.

“Ni furaha isiyo kifani kwangu hasa ikizingatiwa ubabe, uzoefu na tajriba ya wapinzani wangu,” akatanguliza Kigen ambaye ni mzaliwa wa Kaunti ya Baringo.

Kukamilika kwa mbio hizo kulipisha kivumbi cha mita 5,000 kwa upande wa wanawake ambacho kilitawaliwa na Kasait kwa muda wa dakika 15:33.63.

Mshindi huyu wa nishani ya shaba katika mbio za Nyika Duniani mnamo 2017 aliwaonyesha vumbi Waethiopia Feysa Hawi na Tariku Alemitu walioandikisha muda wa dakika 15:33.99 na 15:37.15 mtawalia.

Mkenya mwingine aliyekuwa akishiriki mbio hizo, Lydia Jeruto Lagat aliambulia nafasi ya sita kwa muda wa dakika 15:43.56.

Kigen na Kasait waliwezesha Kenya kutetea ubingwa wa fani hizo ilizozitawala jijini Brazzaville, Congo mnamo 2015 kupitia kwa Clement Kemboi na Margaret Chelimo mtawalia.

Kwa mujibu wa Kipruto, kujiondoa kwake katika mbio hizo kulichochewa na haja ya kujihadhari kutokana na jeraha la mguu ambalo amekuwa akiliuguza kwa muda.Ingawa hivyo, alikiri kwamba mbio za Rabat zilimpa jukwaa la kujiandaa vyema kwa Riadha za Dunia ambazo anapania kuzitamalaki kadri anavyojizatiti kutetea ufalme wa fani ya kuruka maji na viunzi jijini Doha, Qatar baadaye mwezi ujao.

“Mnamo Jumamosi, sikukimbia tena jinsi ilivyotarajiwa na wengi katika Riadha za Diamond League jijini Paris, Ufaransa. Sawa na wakati huo, nilihisi tena maumivu kwenye bega na nikalazimika kujihadhari,” akasema Kipruto ambaye alikuwa mwingi wa sifa kwa Kigen.

Awali katika mbio za mita 400 kwa upande wa wanawake, Mary Moraa wa Kenya alifuzu kwa raundi ya pili ya mchujo baada ya kuandikisha muda wa sekunde 52.31 na kumpiku Mganda Shida Leni aliyefika utepeni baada ya sekunde 53.31.

Linda Kageha aliandikisha muda wa sekunde 54.12 katika mchujo mwingine na kujikatia tiketi ya kusonga mbele licha ya kuzidiwa maarifa na Beatrice Masilingi wa Namibia.

Syombua aondolewa mapema

Hellen Syombua aliondolewa mapema baada ya kukamilisha mchujo wake katika nafasi ya saba kwa muda wa sekunde 58.83. Kwa upande wa wanaume, Alphas Kishioyan aliandikisha muda wa sekunde 46.46 na kufuzu kwa raundi ya pili kwa pamoja na Ditiro Nzamani na Joseph Orukpe wa Botswana.

Kipruto aliyekuwa akishiriki Diamond League kwa mara ya kwanza tangu ashinde fainali ya 2018 mnamo Agosti 30 jijini Zurich nchini Uswizi akiwa na kiatu kimoja, alikamilisha mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji nchini Ufaransa mwishoni mwa wiki jana katika nafasi ya tano.

El Bakkali alitwaa taji kwa dakika 8:06.64 akifuatwa na Kigen (8:07.09) na Waethiopia Lamecha Girma (8:08.63) na Chala Beyo (8:09.36) kabla ya Kipruto ambaye pia ni bingwa wa Afrika na Jumuiya ya Madola kuvuka laini ya kumalizia mbio kwa dakika 8:13.75.

Wakenya wengine walioshiriki mbio hizo ni Nicholas Kiptanui, Abraham Kibiwot, Amos Kirui, Lawrence Kipsang na Wilberforce Kones waliomaliza katika nafasi za sita, tisa, 11, 13 na 16 naye Barnabas Kipyego alijiondoa kabla ya kufika mwisho.

You can share this post!

Aliyekuwa mwenyekiti TLB afariki kutokana na kansa

‘Mikebe ya plastiki badala ya kutupwa ovyo yaweza...

adminleo