Michezo

Fainali ya Chapa Dimba Mt Kenya kupigwa wikendi

January 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

JEFF KINYANJUI na JOHN ASHIHUNDU

MASHINDANO ya mzunguko ya michuano ya kuwania taji la Chapa Dimba na Safaricom nchini, wikendi hii yatafanyika Nanyuki Stadium kuamua mshindi wa eneo la Kati.

Bingwa mpya wa kanda hiyo kwa timu za wavulana atapatikana baada ya watetezi Euronuts kutoka Kaunti ya Kiambu kubanduliwa katika hatua ya makundi.

Barcelona ya Kaunti ya Laikipia, ambayo imebadilisha jina na kujiita Falling Waters, itatetea taji la wasichana baada ya kutinga fainali kwa mara nyingine.

“Tunafurahia kurejea kwa mara nyingine kutambua vipaji mashinani kupitia kwa mashindano haya, huku nikitoa mwito kwa mashabiki wa tabaka zote wajitokeze kwa wingi kushuhudia mashindano kesho na Jumapili,” alisema Mshirikishi wa michuano hiyo ya Kanda ya Kati, Naaman Amboka.

Jumla ya timu nane zimefuzu kwa fainali hizo, nne za wavulana ambazo ni; Irigiro FC kutoka Maragua, Jysa ya Juja, Ulinzi Youth ya Nanyuki na Kiamutugu Boys kutoka Kirinyaga. Timu za wasichana ni Limuru Starlets (Kiambu), Achievers Queens ya Ruiru (Kiambu), Falling Waters ya Nyahururu (Laikipia) na Karima Queens ya Nyeri.

Mshindi wa Kanda atapokea Sh200,000, mbali na fursa ya kuwakilisha eneo la Kati katika fainali za kitaifa. Timu zitakazomaliza katika nafasi ya pili zitapewa Sh100,000, mbali na zawadi kemkem vikiwemo vikombe kutoka kwa wadhamini, Safaricom.

“Kama ilivyo kwa kanda zingine, tumejiandaa vilivyo kwa fainali za Kanda ya Kati, hali ya uchukuzi ni shwari, kuna hoteli za kutosha kuhudumia wachezaji na viongozi wao, huku tukitarajia biashara kuvuma wakati mashindano hayo yakiendelea.

Tayari, Berlin FC ya Garissa kutoka Kaskazini Mashariki, Yanga FC ya Malindi (Kanda ya Pwani) na Kwale Ladies pia ya Pwani zimefuzu kwa fainali za kitaifa huku zikisubiri kuwania tuzo ya Sh1 milioni.