• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 9:50 AM
Faini ya mamilioni na kifungo cha mwaka kwa Mourinho

Faini ya mamilioni na kifungo cha mwaka kwa Mourinho

NA AFP

MADRID, UHISPANIA

KOCHA Jose Mourinho amekubali kifungo cha mwaka mmoja kwa kukwepa ulipaji wa ushuru, mahakama ya Uhispania ilithibitisha hapo jana, ingawa mkufunzi huyo wa zamani wa klabu ya Real Madrid na Manchester United hatahudumia kifungo chochote gerezani baada ya kulipa faini.

Viongozi wa mashtaka walisema kocha huyo alifanya makosa hayo kati ya 2011 na 2012, alipokuwa akiandaa klabu ya Real Madrid “kwa lengo la kupata faida kwa njia haramu”.

Pamoja na hukumu ya mwaka mmoja, Mourinho amepigwa faini ya Sh20.8 milioni ambazo ni asilimia 60 ya pesa zilizopotea.

Hata hivyo, kocha huyo mwenye umri wa miaka 56 hakuweza kufikiwa, Mourinho ni mingoni mwa makocha walio na ufanisi mkubwa duniani, akikumbukwa kwa kuisaidia Chelsea kutwaa mataji kadhaa akiwa kocha, Inter Milan, Real Madrid na FC Porto ya Ureno.

Kadhalika aliisaidia Porto kutwaa ubingwa wa Klabu Bingwa barani Ulaya (UEFA) mnano 2004 na pia 2010 akiwa na Inter Milan ya Italia.

Alitimuliwa na Manchester mwezi Desemba kufuatia matokeo duni kwenye mechi za Ligi Kuu nchini Uingereza (EPL).

Katika habari nyingine kama hiyo, staa Cristiano Ronaldo alikubali kulipa faini ya Sh2.1 bilioni ili kuepuka kufungwa kuhusiana na kesi ya mapato.

Ronaldo alitenda kosa hilo mnamo 2010 na 2014 wakati ambapo Mourinho alikuwa akiinoa Madrid.

Mwenzake Xabi Alonso pia wa Madrid vilevile alikabiliwa na mashtaka ya ukwepaji kodi ya Sh457 milioni lakini akakanusha mashtaka hayo.

Marcelo Vieira alikubali kifungo cha nje cha miezi minne kwa kutumia makampuni ya ughaibuni kushughulikia mapato yake ya Sh28.8 milioni.

Nyota wa Barcelona, Lionel Messi na Neymar ambaye sasa yuko na PSG pia waliwahi kujikuta matatani nchini Uhispania kutokana makosa ya kukwepa kulipa kodi.

Wakati huo huo, imeripotiwa majuzi kwamba Mourinho anakaribia kuajiriwa na klabu ya Paris Saint-Germain (PSG) inayopanga kumtimua Thomas Tuchel licha ya klabu hiyo kuendelea kuongoza msimamo wa ligi kuu ya Ufaransa.

Kinachowafanya wakuu wa klabu hiyo kuamua kutengana na Tuchel ni matokeo mabaya katika michuano ya Klabu Bingwa barani Ulaya.

Imethibitishwa kwamba Mourinho alikutana na Rais wa PSG, Ali Khelaifi akiwa ziarani nchini Qatar majuzi.

Mkutano wao uliwazuzua mashabiki wengi ambao wangependa klabu hiyo ipate mtu anayefaa kabla ya ratiba ijayo ya michuano ya Klabu Bingwa.

Katika juhudi za kuimarisha kikosi chao, PSG wanalenga nyota kadhaa wakiwemo Idrissa Gueye wa Everton, kiungo Frenkie De Jong ambaye pia anawindwa na FC Barcelona pamoja na Marouane Felaini.

You can share this post!

Sare yaletea Liverpool mchecheto ligi ikipamba moto

Kaunti 21 zaitwa kusuluhisha zogo la wauguzi

adminleo