• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 1:24 PM
Farah kukosa mbio za mita 5,000 katika Olimpiki za Tokyo

Farah kukosa mbio za mita 5,000 katika Olimpiki za Tokyo

Na MASHIRIKA

BINGWA mara nne wa Olimpiki, Mo Farah, amethibitisha kwamba hatakuwa sehemu ya wanariadha watakaonogesha mbio za mita 5,000 kwenye Michezo ya Olimpiki itakayoandaliwa jijini Tokyo, Japan mnamo 2021.

Tangazo hilo la Farah linatazamiwa kuwapa Wakenya motisha zaidi ya kuzitamalaki mbio hizo.

Tangu mwaka wa 2005 ambapo Benjamin Limo alitawala mbio hizo katika Riadha za Dunia jijini Helsinki, Finland, Kenya haijawahi tena kunyakua medali ya dhahabu katika fani hiyo ambayo imekuwa ikitamalakiwa na Kenenisa Bekele wa Ethiopia na Mo Farah kwa zaidi ya miaka 10 sasa.

Rekodi ya Kenya katika mbio hizo hata kwenye Michezo ya Olimpiki haijawa ya kuridhisha katika miaka 30 iliyopita.

John Ngugi ndiye Mkenya wa mwisho kuwahi kutia kapuni nishani ya dhahabu katika mbio hizo kwenye Olimpiki za Seoul, Korea Kusini mnamo 1988.

Farah, 37, aliibuka mshindi wa nishani ya dhahabu katika mbio za mita 5,000 na mita 10,000 kwenye Olimpiki za London 2016 na Rio 2016 kabla ya kuelekeza makini yake kwenye mashindano ya marathon.

Hata hivyo, ameshikilia kwamba atalenga kuhifadhi ufalme wake kwenye mbio za mita 10,000 nchini Japan.

“Naendelea vizuri na maandalizi, ila nadhani muhimu zaidi ni kumakinikia fani moja na kuona ni nini ninachoweza kufanya,” akasema Farah.

Akitangaza marejeo yake kwenye mbio za masafa ya kadri, Farah alivunja rekodi ya dunia kwa kukimbia umbali wa mita 21,330 chini ya saa moja kwenye kivumbi cha Diamond League kilichoandaliwa jijini Brussels, Ubelgiji mnamo Septemba 4, 2020.

Baada ya ufanisi huo, alitawala Nusu Marathon ya Antrim Coast nchini Ireland ya Kaskazini mnamo Septemba 12 na akakaribia kuvunja rekodi yake mwenyewe kwenye mbio hizo za kilomita 21.

“Bila shaka napata motisha tele. Nina kiu ya kutia kapuni mataji zaidi,” akasema kwa kufichua kwamba anapania kuweka rekodi ya kuwa mwanariadha wa kwanza katika historia kuibuka mshindi wa medali ya dhahabu katika mbio za mita 10,000 kwenye Olimpiki tatu mfululizo.

“Itakuwa historia japo tayari nimeweka historia katika fani mbalimbali ambazo nimeshiriki kwenye ulingo wa riadha hadi kufikia sasa. Kwa mfano, nimekuwa Mwingereza wa kwanza kuibuka mshindi wa dhahabu kwenye Olimpiki mbili mfululizo.”

“Lazima niendelee kufurahia ninachokifanya, nikitabasamu na kuonea tija na fahari mafanikio yangu. Japo haya ninayoazimia kufanya ni magumu, naamini kwamba hakuna lisilowezekana,” akasema.

Mojawapo ya sababu zinazomsukuma kuweka historia katika Olimpiki ni haja ya kuwapa motisha zaidi wanariadha chipukizi wa kizazi hiki.

“Hakuna kisichowezekana iwapo utajitahidi. Nakumbuka nikiwa mtoto mdogo, baada ya kutoka Somalia nikiwa na umri wa miaka minane pekee, bila kufahamu hata neno moja la Kiingereza. Mtu angaliniambia wakati huo kwamba ningalitambuliwa na Malkia wa Uingereza na kuitwa ‘Sir Mo Farah’, basi ningalimshtumu kwa kunitania.”

Mnamo Februari 2020, Farah ambaye ni bingwa mara sita wa dunia, alikashifiwa pakubwa kwa uhusiano wake na aliyekuwa kocha wake Alberto Salazar aliyepigwa marufuku kwa kujihusisha na matumizi ya pufya.

Hata hivyo, Farah alisema kwamba kashfa za aina hiyo ni suala la kawaida katika mchezo.

“Hutakosa wakosoaji. Ukifaulu na ukishindwa kufaulu katika chochote unachokifanya. Uvumi kama huo wa kushiriki matumizi ya dawa za kusisimua misuli ni jambo ambalo mwanamichezo yoyote anaweza kukabiliwa nalo,” akaongeza.

TAFSIRI: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Gor Mahia kusalia na taji la Ligi Kuu baada ya SDT...

Wabunge waitaka serikali ikomeshe mauaji Samburu