Fernandes atawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka 2019-20 kambini mwa Man-United
Na MASHIRIKA
KIUNGO Bruno Fernandes, 26, ametawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka wa 2019-20 kambini mwa Manchester United.
Nyota huyo raia wa Ureno alisajiliwa na Man-United mnamo Januari 2020 na ujio wake ukawa kiini cha ufufuo wa makali ya kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) chini ya kocha Ole Gunnar Solskjaer.
Kurejea kwa Man-United kushiriki soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu wa 2020-21 ni zao la mchango mkubwa wa Fernandes aliyesajiliwa kutoka Sporting Lisbon kwa kima cha Sh9.5 bilioni.
Kuja kwa Fernandes umekuwa kiini cha ufufuo wa makali ya Man-United ambao kwa sasa wameanza kuhisi ukubwa wa mchango wa kiungo Paul Pogba kila anapowajibishwa naye kwenye safu ya kati.
Hadi alipochezeshwa kwa mara ya kwanza kambini mwa Man-United katika mechi iliyowakutanisha na Wolves mnamo Februari 1, 2020, kikosi cha Solskjaer kilikuwa katika nafasi ya nane jedwalini huku pengo la alama 14 likitamalaki kati yao na Leicester waliokuwa ndani ya mduara wa tatu-bora.
Fernandes alituzwa baada ya kupigia asilimia 35.5 ya kura na kumbwaga mshabuliaji Anthony Martial aliyejizolea asilimia 34 ya kura za mashabiki wa Man-United.
Marcus Rashford aliambulia nafasi ya tatu kwa asilimia 10 ya kura huku chipukizi Mason Greenwood akiridhika na nafasi ya nne kwa asilimia 8.4 ya kura.
Sajili wapya Aaron Wan-Bissaka na Harry Maguire walipata asilimia 3.8 na 2.4 ya kura mtawalia.
Katika msimu wa 2019-20, Fernandes alichezeshwa na Man-United katika jumla ya mechi 22 kwenye mapambano yote na akafunga mabao 12. Aidha, ushawishi wake ugani ulihisika pakubwa na akawezesha waajiri wake kutinga nusu-fainali za Kombe la FA, Carabao Cup na Europa League.
Kwa upande wake, Martial, 24, alifungia Man-United jumla ya mabao 23 kutokana na mechi 48 katika mashindano yote nchini Uingereza na bara Ulaya. Rashford alifunga mabao 22 na kuchangia mengine 11 kutokana na jumla ya michuano 44.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO