• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Fifa yabuni hazina ya kulinda masilahi ya wachezaji soka

Fifa yabuni hazina ya kulinda masilahi ya wachezaji soka

Na CHRIS ADUNGO

WANASOKA wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) ambao hawajakuwa wakipokea mishahara kwa muda mrefu kutoka kwa waajiri wao huenda wakapata afueni hivi karibuni.

Hii ni baada ya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) na Muungano wa Wanasoka Duniani (Fifpro) kubuni hazina ya kifedha ya Fifa FFP itakayokuwa ikishughulikia masilahi ya wachezaji ambao hawajakuwa wakilipwa au ambao dalili zote zinaashiria kwamba hawatawahi kulipwa na klabu zao duniani.

FIFA imetenga kima cha Sh1.6 bilioni ambazo zitatiwa katika hazina ya Fifa FFP hadi mwisho wa 2022 ambapo mgao wa fedha hizi utashuhudiwa.

Sh300 milioni zitatumiwa mnamo 2020, Sh400 milioni mnamo 2021 na Sh400 milioni mnamo 2022. Sh500 milioni zitakazosalia katika hazina hiyo zitatumiwa kushughulikia malimbikizi ya mishahara ambayo wachezaji wa vikosi mbalimbali hawajalipwa kati ya Julai 2015 na Juni 2020.

“Kubuniwa kwa hazina hii kumechochewa na haja ya kushughulikia masilahi ya wanasoka ambao hawawezi kwa sasa kujikimu kimaisha kutokana na changamoto mbalimbali za kifedha zinazokabili waajiri wao duniani,” akasema Rais wa FIFA, Gianni Infantino.

Maamuzi ya kubuniwa kwa hazina ya Fifa FFP itakayoanza kutekelezwa mnamo Julai 1, 2020 ni nafuu kubwa kwa wengi wa wachezaji na maafisa wa benchi za kiufundi ambao wanasubiri kulipwa mishahara yao na klabu mbalimbali za KPL.

Hadi kufikia Disemba 2019, Gor Mahia ambao ni mabingwa watetezi na washindi mara 18 wa taji la KPL walikuwa bado hawajawalipa wachezaji wao malimbikizi ya mishahara ya takriban miezi sita.

SoNy Sugar walioondolewa kwenye KPL kwa kukosa mechi tatu kutokana na uchechefu wa fedha, hawakuwa wamelipa mishahara ya wachezaji wao kwa kipindi cha miezi saba.

Matatizo sawa na hayo kwa sasa yanawakodolea macho Kariobangi Sharks na mabingwa mara 13 wa KPL, AFC Leopards.

“Zaidi ya klabu 50 kutoka kwa mataifa 20 duniani zimesambaratika chini ya kipindi cha miaka mitano iliyopita kutokana na uchechefu wa fedha. Hili ni tukio ambalo limewaathiri mamia ya wanasoka,” akasema Rais wa Fifpro, Philippe Piat.

You can share this post!

Shida kivukoni kufuatia feri 2 kuondolewa

Huyo Mo Farah sio tishio tena, yasema AK

adminleo