FKF kupea timu 102 mipira
Na GEOFFREY ANENE
JUMLA ya klabu 102 zitanufaika na mradi wa kupewa mipira ya kuchezea kutoka kwa Shirikisho la Soka Kenya (FKF) kabla ya msimu mpya kung’oa nanga.
Taarifa kutoka kwa FKF zinasema kuwa shirikisho hilo linapanga kupeana mipira 1,600 katika shughuli hiyo iliyoanza Septemba 30 katika makao yake makuu katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani jijini Nairobi na kuratibiwa kukamilika Oktoba 2.
Katika siku ya kwanza ya shughuli hiyo, FKF ilithibitisha kuwa tayari klabu 18 zinazoshiriki Ligi Kuu ya Wanaume zilipokea mipira 20 kila moja. Siku ya Alhamisi ilikuwa zamu ya timu 16 kutoka Ligi Kuu ya Wanawake na 16 kutoka Ligi ya Daraja ya Pili ya Wanawake. Kila timu kutoka ligi hizo za wanawake ilipokea mipira 20 na 10, mtawalia.
Klabu 32 zinazoshiriki Ligi ya Daraja ya Tatu ya Ukanda ‘A’ na ‘B’ zitanufaika na msaada huo hapo Ijumaa. Zitapokea mipira 10 kila timu.
Klabu 20 kutoka Ligi ya Daraja ya Pili ya Wanaume (NSL) zitapokea mipira 20 kila timu kujiandaa kwa msimu wa 2020-2021 ambao bado haujajulikana utaanza lini. Soka haijaondolewa kwenye orodha ya michezo iliyopigwa marufuku ili kuzuia mikusanyiko inayoweza kuchangia katika uenezaji wa virusi hatari vya corona.
Virusi hivyo vimeua watu 718 nchini Kenya na 1,019,917 dunia nzima. Michezo isiyo ya kugusana ikiwemo riadha imesharejelewa baada ya kusimamishwa mwezi Machi. Soka iko katika orodha ya michezo ‘hatari’ kwa sababu wachezaji hugusana wanapokuwa mazoezini ama kwenye mashindano.