• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:27 PM
FKF kushtakiwa kwa kukosa kulipa Starlets

FKF kushtakiwa kwa kukosa kulipa Starlets

Na CHRIS ADUNGO

WANASOKA wa Harambee Starlets walioshiriki fainali za Cecafa 2018 wamewasilisha malalamishi yao kwa Shirika la Haki za Binadamu la Rigena kwa matumaini kwamba litashinikiza Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) kuwalipa marupurupu ya kushiriki kivumbi hicho nchini Rwanda.

Madai hayo ndiyo ya hivi karibuni zaidi dhidi ya FKF ambayo pia inakabiliana na mizozo ya uchaguzi wa viongozi wapya na madeni ya wakufunzi wa zamani wa Harambee Stars – Adel Amrouche, Sebastien Migne na Bobby Williamson.

Rigena wamekiri kupokea malalamishi dhidi ya FKF na wataanzisha kesi kwa niaba ya wanasoka hao wa Starlets huku wakishinikiza shirikisho kutoa malipo yanayodaiwa na wachezaji hao tangu 2018.

“Ni kinyume cha haki kwa shirikisho lililoanzishwa kwa misingi ya sheria kuwatumia vibaya wasichana walio katika uhitaji mkubwa na kupuuza wanapodai kulipwa,” ikasema sehemu ya barua ya iliyowasilishwa na Rigena kwa FKF. Barua hiyo ilitiwa saini na mwenyekiti wa Rigena, Thomson Kerongo.

“Hatua ya FKF inawaweka wanasoka wengi katika hofu zaidi. Tunaamuru FKF iwalipe wanasoka wote wa Starlets wanaoidai kutokana na fainali za Cecafa 2018 haraka iwezekanavyo chini ya kipindi cha siku 14 zijazo na iache kuwatishia wachezaji waliowasilisha malalamishi hayo,” ikaendelea barua hiyo.

“Iwapo hatutapokea jibu la kuridhisha kutoka FKF, hatutasita kutafuta haki mahakamani, bila ya kuhusisha, FKF kwa minajili ya kupigania maslahi ya wachezaji husika,” ikasema barua.

Kwa mujibu wa Rigena, FKF imekuwa ikilazimika kuita kambini wanasoka wapya kila mara wachezaji wa Starlets waliowajibishwa 2018 wanapotoa masharti ya kulipwa mwanzo kwa marupurupu yao ya awali kabla ya kuchezeshwa katika vibarua vingine. Kila wanapogomea FKF, wanasoka hao wamekuwa wakitishwa na hatimaye kutemwa kikosini.

Hadi kufikia sasa, wanasoka hao wa Starlets walioshiriki Cecafa 2018 wamelipwa na FKF Sh15,000 pekee na bado wanadai salio la Sh120,000 kila mmoja.

 

  • Tags

You can share this post!

Imani tele fedha za bajeti zitainua vijana kispoti

Huenda Gor ikapoteza mastaa sita

adminleo