FKF yaomba Starlets wacheze COSAFA
Na GEOFFREY ANENE
SHIRIKISHO la Soka Kenya (FKF) limeandikia barua Baraza la Soka la mataifa ya Kusini mwa Afrika (COSAFA) kuomba timu ya taifa ya soka ya wanawake ya Kenya almaarufu Harambee Starlets ishiriki mashindano ya mwaka 2020 mjini Nelson Mandela Bay nchini Afrika Kusini mnamo Novemba 3-14.
Mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) Starlets waliwahi kushiriki COSAFA mwaka 2017 na kukamilisha kampeni yao katika nafasi ya nne.
Starlets ililemewa na Shepolopolo ya Zambia katika mechi ya kutafuta mshindi wa medali ya shaba kwa njia ya penalti 4-2 baada ya muda wa kawaida kukamilika 1-1 ambapo Neddy Atieno (Kenya) na Barbra Banda (Zambia) waliona lango.
Warembo wa kocha David Ouma walikuwa wamezaba Msumbiji 5-2, Mauritius 11-0 na Swaziland 1-0 katika mechi za makundi kabla ya kuchapwa 4-0 na Zimbabwe katika nusu-fainali.
Kenya ingali inasubiri jibu kutoka kwa COSAFA, ingawa baraza hilo limethibitisha katika tovuti yake kuwa FKF imeomba Starlets ipewe nafasi kushiriki mashindano hayo.
Baraza hilo limesema kuwa Afrika Kusini, Zambia, Zimbabwe, Komoro, Angola na Malawi zimetoa ithibati ya kushiriki, huku timu za Namibia na Eswatini (Swaziland) zikisubiri idhini kutoka kwa serikali kuhusu usafiri kutokana na masharti yaliyowekwa ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.
“Mauritius bado haijulikani kama itashiriki. Madagascar, Ushelisheli na Msumbiji zimesema hazitashiriki mashindano ya COSAFA mwaka huu. Lesotho haijatangaza msimamo wake,” COSAFA iliongeza.
Starlets imesakata mechi tatu pekee mwaka 2020. Ilialikwa nchini Uturuki kushiriki Kombe la Uturuki mwezi Machi ambapo ilipepeta Northern Ireland Under-19 kwa mabao 2-0 kabla ya kupoteza dhidi ya Chile 5-0 na Ghana 3-1 katika mechi za Kundi B mjini Alanya.
Kenya ilifaa kumenyana na Tanzania nyumbani na ugenini mwezi Aprili katika mechi za raundi ya kwanza za kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AWCON) 2020, lakini makala hayo yakafutiliwa mbali kutokana na janga la corona.
Starlets iliteremka nafasi nne hadi nambari 137 duniani kwenye viwango bora vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) vilivyotangazwa mwisho hapo Agosti 14.