Michezo

FKF yatoa ratiba ya uhamisho wa wachezaji katika ligi ndogo

September 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

KLABU zinazoshiriki soka ya Ligi Kuu ya Wanawake humu nchini (KWPL) na Ligi ya Daraja la Kwanza ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), zimepata idhini ya kujisuka upya kwa minajili ya msimu ujao kuanzia Jumanne ya Septemba 8, 2020.

Muhula wa uhamisho wa wachezaji katika KWPL umepangiwa kukamilika rasmi mnamo Novemba 16 huku ule wa Daraja la Kwanza ukiwa umeratibiwa kuanza Septemba 14 hadi Novemba 23.

FKF inatarajiwa kutoa ratiba kamili ya michuano ya muhula huu katika ligi mbalimbali za soka ya humu nchini pindi serikali itakapoondoa baadhi ya masharti yaliyowekwa katika juhudi za kudhibiti msambao wa ugonjwa wa Covid-19.

Kwingineko, mabingwa mara 19 wa Ligi Kuu ya KPL, Gor Mahia wamewapiga kumbo AFC Leopards katika vita vya kumsajili fowadi matata mzawa wa Burundi, Jules Ulimwengu, 21.

“Yalikuwa matamanio yangu kuingia katika sajili rasmi ya Leopards. Hata hivyo, wakala wangu alinishawishi kubadilisha msimamo na ilivyo, dalili zote zinaashiria kwamba nitakuwa mchezaji wa Gor Mahia,” akasema chipukizi huyo katika mahojiano yake na Taifa Leo.

Ujio wa Ulimwengu kambini mwa Gor Mahia unatazamiwa kumpa jukwaa bora la kushirikiana vilivyo na fowadi mahiri mzawa wa Uganda, Tito Okello aliyesajiliwa na miamba hao hivi majuzi kutoka Vipers SC.

Hadi kufikia sasa, Gor Mahia wamejinasia huduma za wanasoka 10 baada ya kuagana rasmi na wachezaji saba – Joash Onyango (Simba SC), David Mapigano (Azam FC), Dickson Ambundo (Dodoma Jiji), Boniface Omondi na Peter Odhiambo (Wazito FC), Juma Balinya (KCCA) na Jackson Owusu.

Kikosi hicho cha kocha Steven Polack kinatazamiwa pia kukatiza uhusiano na kiungo Lawrence Juma na beki Charles Momanyi wanaohusishwa na uwezekano mkubwa wa kujiunga na Sofapaka na KCB mtawalia.

Momanyi anahemewa pia na Nairobi City Stars ambao tayari wamesajili beki Ronny Kola Oyaro, 20, Rowland Makati (Vapor Sports) na chipukizi wa Laiser Hill Academy, Timothy Ouma.

Baadhi ya sajili wapya kambini mwa Gor Mahia ni Benson Omalla, Sydney Ochieng, Samuel Njau, Kelvin Wesonga, John Ochieng, John Macharia, Bertrand Konfo kutoka Cameroon na Andrew Malisero Numero ambaye ni mzawa wa Malawi.