FKF yatoa tarehe ya mchujo kati ya Nairobi Stima, Posta
Na CHRIS ADUNGO
NAIROBI Stima watakuwa wenyeji wa Posta Rangers katika mchuano wa mkondo wa kwanza wa mchujo wa kubaini kikosi kitakachofuzu kwa Ligi Kuu ya KPL msimu ujao mnamo Juni 15 ugani Karuturi.
Mchuano wa marudiano utaandaliwa na Rangers mnamo Juni 19 katika uwanja wa Kenyatta, Machakos.
Rangers walikamilisha kampeni zao za KPL msimu huu katika nafasi ya 16 mbele ya Vihiga United na Mount Kenya United walioteremshwa ngazi. Kikosi hicho cha mkufunzi John Kamau kilisajili ushindi mara saba, kuambulia sare mara 11 na kupoteza mechi 16 kati ya 34 za msimu huu.
Matokeo hayo yaliwavunia jumla ya alama 32 na hivyo kuwaweka katika nafasi ya 16 kwenye orodha ya wapinzani 18 waliokuwa wakiwania ufalme wa KPL msimu jana.
Ilivyo, kikosi kinachomaliza katika nafasi ya tatu kwenye kampeni za NSL hujikatia tiketi ya kushiriki mchujo dhidi ya kikosi nambari 16 kwenye jedwali la KPL.
Mshindi wa mikondo miwili ya mchujo huo hufuzu kuwania ubingwa wa KPL katika msimu unaofuata huku mpinzani anayezidiwa maarifa akisalia kunogesha kipute cha NSL.
“Stima watakuwa waandalizi wa mchuano wa mkondo wa kwanza wa mchujo wa kuingia KPL dhidi ya Rangers mnamo Juni 15 mjini Naivasha. Vikosi hivyo vitarudiana siku nne baadaye mjijni Machakos,” ikasema sehemu ya taarifa iliyotolewa Jumatano na Shirikisho la Soka la Kenya (FKF).
Wazito FC na Kisumu All Stars waliotawala kampeni za NSL msimu huu tayari wamepandishwa daraja kuwania ubingwa wa KPL muhula ujao. Vikosi hivyo vilichukua nafasi za Vihiga Utd na Mt Kenya Utd walioshushwa ngazi baada ya kukokota nanga mkiani mwa jedwali la KPL kwa alama 26 na 18 mtawalia.
Thika United, Green Commandos na Kangemi All Stars waliteremshwa ngazi kwenye kivumbi cha NSL, na kwa watashiriki Ligi ya Daraja la Kwanza msimu ujao.
Wazito warejea
Wazito waliotemwa kwenye KPL msimu jana, wanarejea kuwania ubingwa wa kipute hicho baada ya kujikusanyia jumla ya pointi 81 kutokana na mechi 38, huku Kisumu All Stars wakimaliza katika nafasi ya pili kwa pointi 80, sawa na Nairobi Stima waliokuwa na mabao machache.
Katika mchuano wao wa mwisho wa msimu huu, Stima walisajili ushindi wa 7-1 dhidi ya wenyeji wao Eldoret Youth ugani Camp Toyoyo.
Amos Asembekha aliwafungia Wazito mabao matatu huku mengine yakipatikana kupitia kwa Joseph Waithaka na Paul Acquah.
Bao la pekee la St Joseph lilifungwa na Kevin Taabu mwishoni mwa kipindi cha pili.
Kiini cha Stima na Rangers kuvaana mapema ni kwa sababu vikosi vyote vya NSL na KPL vinatarajiwa kuanza mapumziko ya takriban wiki tatu kabla ya kuanza mipango ya kujiandaa kwa msimu mpya.
Wakiwapepeta Rangers baada ya mikondo mwili, itakuwa mara ya kwanza kabisa kwa kikosi hicho kuwania ufalme wa KPL. Rangers walioshiriki KPL kwa mara ya kwanza mnamo 2010, walitemwa mnamo 2012 kabla ya kurejea kwa matao ya juu mnamo 2016.