Michezo

FUNGA-KAZI: Muhula wa uhamisho wafungwa rasmi Ulaya

September 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

ILIKUWA ni hekaheka na wingi wa shughuli katika dakika za mwisho miongoni mwa klabu mbalimbali za bara Ulaya hapo jana Jumatatu muhula wa uhamisho wa wachezaji ulipofungwa rasmi.

AS Roma walijitwalia huduma za kiungo matata wa Arsenal na timu ya taifa ya Armenia, Henrikh Mkhitaryan kwa mkopo wa msimu mmoja.

Mkhitaryan alijiunga na Arsenal mnamo Januari 2018 katika tukio lililomshuhudia fowadi wa Chile Alexis Sanchez ambaye kwa sasa yupo Inter Milan kwa mkopo wa mwaka mmoja, akiyoyomea Manchester United.

Hadi kubanduka kwake ugani Emirates, Mkhitaryan alikuwa amewapigia Arsenal jumla ya mechi 59 ikiwemo ya wikendi iliyopita dhidi ya Tottenham Hotspur.

Kuondoka kwake kulichochewa na kauli ya hivi majuzi ya kocha Unai Emery aliyesisitiza kwamba anapangia kuwapa chipukizi wengi zaidi katika academia ya Arsenal nafasi ya kukiwajibikia kikosi hicho.

Arsenal walitarajiwa pia kuagana Jumatatu na beki Shkodran Mustafi, 27, japo nyota huyo wa Ujerumani alikuwa awali amefichua ukubwa wa matamanio yake ya kusalia Emirates.

Kwingineko, Matteo Darmian wa Man-United na timu ya taifa ya Italia alitua kambini mwa Parma kusakata soka ya Serie A nchini Italia kwa mkataba wa miaka minne. Sogora huyo mwenye umri wa miaka 29 alisajiliwa na kocha Louis van Gaal kutoka Torino kwa kima cha Sh1.7 bilioni mnamo Julai 2015.

Hadi kuvunjika kwa ndoa kati yake na Man-United, Matteo alikuwa amewajibishwa mara 92 na aliwasaidia waajiri wake kunyanyua ubingwa wa Kombe la FA mnamo 2015-16.

Ingawa hivyo, alichezeshwa mara saba pekee msimu jana chini ya kocha Ole Gunnar Solskjaer huku akiwajibishwa mara 13 pekee tangu Disemba 2017.

Mkataba wake ugani Old Trafford ulitarajiwa kutamatika mwishoni mwa 2020.

Anakuwa mchezaji wa tano baada ya Chris Smalling (Roma), Sanchez (Inter), Romelu Lukaku (Inter) na Ander Herrera (PSG) kubanduka kambini mwa Man-United muhula huu.

Ilikuwa rahisi zaidi kwa Solskjaer kumwachilia Darmian ambaye alifichua azma yake ya kurejea Italia yapata miezi 12 iliyopita.

Kikosi kingine kilichojishughulisha jana katika soko la uhamisho wa wachezaji ni Napoli SC ambacho kilijinasia huduma za mvamizi mkongwe wa Tottenham Hotspur na timu ya taifa ya Uhispania, Fernando Llorente, 34.

Llorente aliingia katika sajili rasmi ya Spurs mnamo 2017 na aliwafungia miamba hao wa soka ya Uingereza bao la ushindi katika mechi ya robo-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) dhidi ya Manchester City msimu uliopita.

Awali, Llorente alikuwa amekiwajibikia pia kikosi cha Swansea City alichokisaidia kukwepa pigo la kuteremka daraja kwenye Ligi Kuu ya EPL mnamo 2016-17.

Hadi aliposajiliwa na Swansea, Llorente alikuwa pia amewahi kuwachezea Juventus kati ya 2013 na 2015 na kunyanyua mataji mawili ya Ligi Kuu ya Serie A.

Akijivunia kuvalia jezi za timu ya taifa ya Uhispania mara 24, Llorente alihudumu kambini mwa Athletic Bilbao kwa misimu tisa kabla ya kutua Juventus kisha kuyoyomea Sevilla kwa msimu mmoja zaidi. Llorente aliyewasaidia Uhispania kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia mnamo 2010 na Eueo 2012 nusura ajiunge na Chelsea mnamo 2016 chini ya mkufunzi Antonio Conte ambaye kwa sasa anadhibiti mikoba ya Inter Milan.

Atuma barua

Sevilla pia walijinasia jana huduma za mvamizi wa zamani wa Man-United, Javier ‘Chicharito’ Hernandez, 31, kwa mkataba wa miaka mitatu kutoka West Ham United.

Fowadi huyo wa timu ya taifa ya Mexico aliwapa West Ham United chini ya kocha Manuel Pellegrini barua ya kutaka aachiliwe atue Sevilla mwishoni mwa wiki jana.

Kiini cha kuondoka kwake kambini mwa West Ham ni hatua ya kikosi hicho kumsajili nyota Sebastien Haller kutoka Eintracht Frankfurt mnamo Julai 2019.

West Ham walimsajili Chicharito kutoka Bayer Leverkusen ya Ujerumani kwa kima cha Sh2 bilioni mnamo 2017.

Hadi kuondoka kwake jijini London, alikuwa amewachezea West Ham United mara 55 na kufunga jumla ya mabao 16 katika kivumbi cha EPL.

Aidha, miamba wa soka nchini Uturuki, Galatasaray walikamilisha uhamisho wa fowadi Radamel Falcao kutoka AS Monaco nchini Ufaransa.

Falcao, 33, alikuwa na mwaka mmoja katika mkataba wake na Monaco waliomtwaa kutoka Atletico Madrid kwa kima cha Sh6.5 bilioni mnamo 2013. Baada ya kuhudumu kambini mwa Man-United na Chelsea kwa mkopo kati ya 2014 na 2016, alirejea Monaco.

Nyota huyo mzaliwa wa Colombia anajivunia kuifungia Monaco jumla ya mabao 83 kutokana na mechi 139 za Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1).