Furaha riboribo Mathare North ikitwaa Tujiamini Cheza Dimba Nairobi
KOCHA wa Mathare North United David Onyango amesema kuwa kujituma kwa vijana wake ndiko kichocheo kikuu kilichosababisha washinde ubingwa wa Tujiamini Cheza Dimba ukanda wa Nairobi.
Mathare North ilionyesha mchezo ulioenda shule na kutwaa ubingwa huo baada ya kuilemea Planes FC 2-0 katika fainali iliyogaragazwa uga wa Dandora.
Kwa kuibuka washindi, Mathare North United ilijishindia udhamini wa miaka mitatu ambao ni wa kima cha Sh250, 000.
Kwenye mechi ya kwanza, mabingwa hao walipata mabao yao kupitia Ramadhan Otieno na George Ochieng na kuishinda Zimmerman All Stars 2-0.
Katika hatua ya nusu fainali walichapa Indomitable FC 2-0, huku straika Michael Itiyeng aking’aa katika mashindano hayo kwa kutinga magoli matano kati ya tisa ambayo timu yake ilifunga.
“Tulijituma sana kupata ushindi huu kando na kuonyesha mchezo mzuri. Udhamini wa Tujiamini utatusaidia kwa sababu tutanunua baadhi ya vifaa kwa timu yetu na mashindano haya pia yamewawezesha wanasoka wetu watambuliwe,” akasema Onyango.
Itiyeng naye alisema kuwa timu hiyo inayoshiriki Ligi ya Shirikisho la Soka Nchini (FKF) Divisheni ya Kwanza inalenga kujituma sana msimu huu ili watinge Ligi ya Kitaifa (NSL) msimu ujao.
Mwanadimba huyo aliwashukuru wenzake kikosini kutokana na ushirikiano waliokuwa nao uwanjani ambao ulianika talanta zao huku wengi wakitarajia kuchezea baadhi ya klabu za hadhi nchini.
Kocha wa Planes Mathias Ocholi naye aliwashukuru wachezaji wake kwa kutoa upinzani mkali kwa Mathare North akisema wana matumaini ya kutwaa ubingwa siku zijazo.
“Kikosi changu bado ni changa na tutarekebisha makosa yetu ili katika mechi zijazo tupate ushindi,” akasema Ocholi.
Nahodha wa Planes aliwapongeza wenzake kikosini akisema hawakubahatika kupata ushindi ila wana matumaini ya kutamba siku zijazo.
Afisa wa Mawasiliano wa Sportpesa Mercy Kabui alisema kuwa kampuni hiyo itaendelea kufadhili mashindano ya soka kama sehemu yake ya kutambua na kukuza talanta.
“Kama Sportpesa tunastahi katika kuihudumia jamii na kuchangia ufanisi maishani mwa vijana. Lengo letu ni kukuza talanta mashinani ili kuwe na wanasoka wakali hata katika kiwango cha juu cha soka,” akasema Kabui.
Makala yafuatayo ya Cheza Dimba inaelekea Nyanza wikendi hii