• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Gaspo wafichua malengo yao ya msimu huu ligini baada ya kusajili wavamizi wa haiba kubwa

Gaspo wafichua malengo yao ya msimu huu ligini baada ya kusajili wavamizi wa haiba kubwa

Na CHRIS ADUNGO

GASPO FC wanaoshiriki Ligi Kuu ya Kenya (KWPL) wanatarajia msimu wa kuridhisha utakaowavunia idadi kubwa zaidi ya mabao muhula huu hasa ikizingatiwa ubora wa viwango vya mafowadi wapya waliojiunga nao msimu huu.

Meneja wa timu hiyo, Edward Githua anaamini kwamba sajili wapya kambini mwao wanaleta nguvu mpya, tajriba pevu na uzoefu utakaowawezesha kuwapokonya Vihiga Queens ubingwa wa taji hilo muhula huu wa 2020-21.

“Tumesajili idadi kubwa ya wanasoka wa haiba ambao naamini watatukweza pazuri katika kampeni za msimu huu. Kikosi kiko tayari kwa kibarua kilichopo mbele na tunatazamia kuanza vyema na kuibuka mabingwa hatimaye,” akasema Githua.

Miongoni mwa washambuliaji wazoefu zaidi waliongia kambini mwa Gaspo FC muhula huu ni Stella Liseche kutoka Kibera Girls Soccer Academy na Rhoda Nafula wa Wiyeta. Diana Wacera anarejea pia kikosini mwa Gaspo baada ya kuagana na Mathare waliomwaminia utepe wa unahodha.

Mbali na hao, Gaspo walijinasia pia maarifa ya aliyekuwa fowadi matata wa Kisumu Starlets, Mercy Airo aliyepachika wavuni mabao 30 katika msimu wa 2019-20 na kuambulia nafasi ya pili kwenye orodha ya wafungaji bora ligini.

Hata hivyo, Githua anatarajia ushindani mkali kutoka kwa wapinzani wao wakuu hasa mabingwa wa 2017, Thika Queens ambao wamesajili jumla ya wanasoka 15 wapya.

Gaspo wameratibiwa kuvaana na Zetech Sparks katika mchuano wao wa kwanza wa msimu uwanjani Ruiru mnamo Disemba 12, 2020.

Jumla ya vikosi sita (tatu kutoka kila zoni) zitafuzu kwa mchujo wa kutafuta mshindi wa taji la Ligi Kuu msimu huu.

  • Tags

You can share this post!

Gor Mahia kukutana sasa na CR Belouizdad ya Algeria katika...

Lukaku afunga na kusaidia Inter kuangusha Bologna ligini