Michezo

Gaya kuongoza kikosi cha Kenya Morans kinara akitoa wito kwa KBF kumrejesha kocha Cliff Owuor

December 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

COLLINS Gaya aliyekuwa msaidizi wa kocha Cliff Owuor, atasamamia sasa mazoezi ya wanavikapu wa Kenya Morans. Hii ni baada ya Owuor kujiunga rasmi na kikosi cha Rwanda Patriotic Army (APR).

Owuor hakurejea nchini wikendi iliyopita pamoja na kikosi na maafisa wengine wa benchi ya kiufundi wa Morans aliosafiri nao jijini Kigali, Rwanda kwa mechi za raundi ya kwanza za kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AfroBasket) 2021.

Kwa kukubali upya chombo cha APR, Owuor anajerea katika kikosi alichokinoa kwa kipindi cha miaka 15 hadi 2018 alijiunga na wasomi wa Chuo Kikuu cha USIU-A.

Katika mahojiano yake na Taifa Leo, alilalamikia suala la baadhi ya ‘watu wenye ushawishi’ kuingilia pakubwa shughuli ya kuteuliwa kwa wachezaji wa kuunga timu ya taifa ya Morans – jambo ambalo amekiri lilivuruga utendakazi wake na kumnyima fursa ya kuwa na usemi katika harakati za kuwajibikia kikosi.

“Morans ni miongoni mwa vikosi bora zaidi vya vikapu barani Afrika. Ni timu inayojivunia idadi kubwa ya wachezaji wenye uwezo wa kutwaa mataji ya haiba kubwa iwapo tu shughuli za benchi ya kiufundi hazitatizwa na ‘watu wenye maslahi binafsi’. Hilo ndilo donda sugu ndani ya Morans,” akasema kwa kukiri kwamba amekuwa akiwaniwa na APR tangu Agosti mwaka huu.

Owuor pia alilalamikia suala la kutokuwepo kwa ushirikiano mzuri kati ya wadau wa mchezo wa vikapu nchini Kenya, akitoa mfano wa jinsi kutotolewa mapema kwa fedha za kikosi kulivyochelewesha safari za baadhi ya wachezaji wa ughaibuni.

“Ipo haja kwa wanavikapu wa nje kuwezeshwa kuripoti kambini kwa wakati ufaao ili kocha aoanishe mitindo ya kucheza kwao na wa wanavikapu wengine wa nyumbani. Hilo likifanikishwa, basi Kenya itakuwa miongoni mwa vikosi vya kutisha zaidi barani,” akaongeza.

Kwa upande wake, Gaya amesema: “Hatuwezi kusubiri zaidi kwa Shirikisho la Vikapu la Kenya (KBF) kutafuta kocha mpya. Kuna kazi kubwa ya kufanywa na kitu bora zaidi cha kufanya ni kuanza mazoezi baada ya wiki moja ya kupumzika.”

Hata hivyo, Peter Orero ambaye alikuwa mkurugenzi wa kikosi cha Morans kwenye mashindano ya kufuzu kwa AfroBasket jijini Kigali, ametaka KBF kufanya hima na kumshawishi Owuor kurejea nchini kuendelea na majukumu yake kambini mwa Morans.

Chini ya Owuor, Morans walipiga Msumbiji 79-62 katika mchuano wa mwisho wa Kundi B na kuweka hai matumaini ya kufuzu kwa fainali za AfroBasket zitakazoandaliwa Rwanda mwakani.

Wanavikapu wa Morans waliingia ugani dhidi ya Msumbiji wakitawaliwa na kiu ya kushinda baada ya chombo chao kuzamishwa na Senegal (92-54) na Angola (83-66) katika mechi mbili za ufunguzi wa Kundi B.

Iwapo Morans watatia fora katika marudiano dhidi ya Angola, Senegal na Msumbiji kwenye mkondo wa pili mnamo Februari 2021 na kutua kileleni mwa Kundi B au kumaliza katika nafasi ya pili, basi watafuzu kwa kunogesha fainali za Kombe la Afrika kwa mara ya kwanza tangu 1993.

Mkondo wa pili ya kipute cha Afro-Basket umeratibiwa kuanza Februari 19, 2021 kwa mechi itakayowakutanisha tena Kenya na Senegal. Baadaye, wanavikapu wa Morans watashuka ugani kukabiliana na Angola mnamo Februari 20 kabla ya kumaliza udhia dhidi ya Msumbiji mnamo Februari 22, 2020.

Kwa mujibu wa orodha ya viwango bora vya kimataifa, Morans ndio wanaokamata nafasi ya chini zaidi kwenye Kundi B. Wanashikilia nambari 122 duniani huku Angola, Senegal na Msumbiji wakiwa katika nafasi za 32, 35 na 93 mtawalia.