Genesis Sports waibuka namba wani kuogelea mbio fupi na relays Kiambu
WAOGELEAJI kutoka klabu ya Genesis Sports Limited waliibuka washindi wa taji la jumla kwenye mashindano ya Kaunti ya Kiambu ya mbio fupi na relays (mbio zinazojumuisha washiriki wanne wanaoogelea backstroke, breaststroke, butterfly na freestyle katika usanjari huo) hapo Machi 22-23, 2025.
Genesis, ambayo ilianzishwa mwaka 2024, ilizoa jumla ya medali 64 (dhahabu 32, fedha 22 na shaba 10) katika shule ya Regis Runda Academy, Kiambu.
Orca SC ilikamata nafasi ya pili kwa dhahabu 28, fedha 25 na shaba 15, nayo Aqua Shark Fin ikafunga tatu-bora kwa dhahabu 19, fedha 12 na shaba 21.
Jumla ya timu 31 kutoka kaunti za Malindi, Meru, Nakuru, Kajiado, Nyeri, Nairobi, Mombasa na Kiambu zilishiriki mashindano hayo yaliyoandaliwa na Chama cha Mchezo wa Kuogelea cha Kaunti ya Kiambu (KCAA).
Baadhi ya timu zilizoshiriki ni Acacia Park School, Aga Khan Academy Nairobi, Crawford International School, Woodcreek School, The Harpoons, Moi Nyeri Complex, Melvin Jones Academy, Loreto Convent Valley Road, Next Gen Multi-Sports Academy, Jawabu School, Gliding Dolphins, Super Marlins SC, Potterhouse School, Thika Marines, Nawiri SC, Seal SC, Beapro SC, na Water Warriors SC.
Katika kitengo cha wasichana walio na umri wa miaka saba kurudi chini cha kuogelea mita 100, Individual Medley, Wanjiru Samara kutoka Genesis aliibuka mshindi akiwa na dakika mbili na sekunde 4.56.
Jed Kahindo kutoka Mombasa Aquatics Club walitawala kitengo cha wavulana kutoka umri wa miaka 10 na 11 cha 100m Individual Medley kwa dakika 1:32.25.
Kahindo alifurahia mashindano, hasa kuona waogeleaji wengi katika kitengo chake na akaahidi kuongeza bidii katika mashindano yajayo.
Alikamilisha kuogelea 400m Freestyle kwa dakika 5:50.00 wakati wa mashindano ya kitaifa ya bwawa fupi mjini Mombasa mwaka jana, 2024.
Mashindano ya bwawa fupi hufanyika katika bwawa la mita 25, huku mashindano ya bwawa refu yakiandaliwa katika bwawa la mita 50.
Chris Kibe kutoka Potterhouse School Runda alishinda kitengo cha 25m backstroke cha wavulana wasiozidi umri wa miaka saba kwa sekunde 39.03.
Nadia Nuru kutoka Aqua Shark Fin aliibuka mshindi wa kitengo 25m cha breastrstroke cha wasichana walio ana umri wa miaka minane hadi tisa kwa sekunde 26.19.
“Mimi hufanya mazoezi makali,” akasema Nuru na kuongeza kuwa anapenda sana kuogelea.
“Nimeweka bidii sana katika kukuza talanta yangu ya breaststroke na ninafurahia matokeo yangu,” akaeleza Nuru.
Kocha Patricia Wanjiru kutoka Jawabu School alishukuru KCAA kwa kuandaa mashindano mazuri na kuongeza kuwa yamesukuma wazazi kuruhusu watoto wao kuogelea baada ya kuona mashindano yaliyopita.
Genesis Sports pia walimaliza kileleni mwa jedwali la wanaume wakiwa na medali 48 (dhahabu 21, fedha 17 na shaba 10) wakifuatiwa na Orca (dhahabu 18, fedha 15 na shaba 10), nao Crawford wakafunga tatu-bora (dhahabu 12, fedha 8 na shaba 12).
Katika kitengo cha wanawake, Potterhouse walihifadhi taji kwa kuzoa medali 28 (dhahabu 12, fedha 6 na shaba 10) wakifuatiwa na Aqua Shark Fin (dhahabu 12, fedha 5 na shaba 10) na Genesis Sports (dhahabu 10 na fedha 5), mtawalia.
Waogeleaji chipukizi walitumia mashindano ya Kiambu kujiweka tayari kwa mashindano ya kitaifa ya chipukizi yatakayoafanyika Mei 3-4 katika shule ya Aga Khan Academy mjini Kisumu.