Ghana yatua nchini ikitarajia kuinyorosha Harambee Stars
Na Geoffrey Anene
BLACK Stars ya Ghana imetua jijini Nairobi Alhamisi jioni kwa mechi ya Kundi F ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2019 dhidi ya wenyeji Harambee Stars hapo Septemba 8, 2018.
Taarifa kutoka Ghana zinasema kwamba Kocha Mkuu wa Black Stars Kwesi Appiah sasa ana kila sababu ya kutabasamu baada ya kikosi chake kukamilika kufuatia kuwasili kwa beki nyota Harrison Afful kutoka klabu ya Columbus Crew SC nchini Marekani hapo Septemba 5.
Appiah na vijana wake walikuwa na kipindi cha mwisho cha mazoezi jijini Addis Ababa nchini Ethiopia mapema Alhamisi, tovuti ya Ghana Guardian imeripoti.
“Black Stars inatarajiwa kutua jijini Nairobi mnamo Alhamisi jioni na kufanya mazoezi katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani kabla ya mechi ya Jumamosi,” tovuti hiyo imesema. Kiungo wa Inter Milan Kwadwo Asamoah, ambaye pia alijiunga na wenzake jijini Addis Ababa kutoka nchini Italia, anatarajiwa kufanywa nahodha licha ya wasiwasi kuhusu fomu yake baada ya kupata jeraha ndogo mazoezini.
Ghana ilituma onyo la mapema kwa wapinzani wake wa Kundi F ilipokung’uta Ethiopia 5-0 katika mechi yake ya ufunguzi mwaka 2018 mjini Kumasi.
Kenya ilianza kampeni yake ya kutafuta kurudi AFCON baada ya miaka 14 kwenye baridi kwa kujikwaa. Ilipepetwa 2-1 na Sierra Leone. Ghana na Sierra Leone zina alama tatu nazo Kenya na Ethiopia zitakuwa zikitafuta alama ya kwanza wikendi hii ya Septemba 8-9.
Ethiopia itaalika Sierra Leone mjini Awassa mnamo Septemba 9. Kenya na Ethiopia zitamenyana mwezi ujao mjini Bahir Dar mnamo Oktoba 10 na jijini Nairobi mnamo Oktoba 14. Mechi mbili za mwisho za Kenya katika kundi hili ni dhidi ya Sierra Leone jijini Nairobi mnamo Novemba 16, 2018 na nchini Ghana mnamo Machi 22, 2019. Timu mbili za kwanza kutoka kila kundi zitaingia AFCON mwaka 2019.