Michezo

Giroud ajitapa atakavyotesa makipa baada ya ujio wa Lampard

July 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA CECIL ODONGO

BAADA ya kutinga mabao mawili kwenye ushindi wa 4-0 dhidi ya St Patrick FC Jumamosi Julai 13 2019, mshambulizi wa Chelsea Olivier Giroud amewaahidi mashabiki wa mabingwa hao wa taji la Uropa kwamba atakuwa moto wa kuotea mbali chini ya mkufunzi mpya Frank Lampard.

Wakati wa mechi hiyo mwanadimba wa Chelsea Mason Mount ambaye awali alikuwa akinolewa na Lampard wakati wa uhamisho wake wa mkopo akisakatia Derby County alifunga bao la kwanza baada ya kupokezwa krosi safi kutoka kwa mlinzi Mateo Kovacic.

Chipukizi Emerson Palmieri aliongeza bao la pili kunako dakika ya 31 kabla ya mabao mengine kufungwa na Giroud katika kipindi cha pili.

Akihojiwa na Radio 5 Live Sports Extra, Giroud alionyesha furaha yake kuhusu ujio wa Lampard ambaye alichukua nafasi ya Maurizio Sarri aliyeyoyomea Juventus ya Italia, akisema dalili za kucheka na nyavu za wapinzani msimu wa 2019/20 sasa ni dhahiri.

“Napenda ari na msukumo wa kushinda kila mechi tunayocheza. Tumekuwa tukifanya mazoezi kabambe yenye kasi ya juu na nimeridhika kwamba Lampard ndiye kocha atakayenipa mshawasha wa kujituma na kufunga magoli. Kwa kuwa ni jagina wa klabu hii, yeye ndiye alistahili kazi hii,” akasema Giroud, ambaye pia alisakatia Ufaransa na kuisaidia kutwaa Kombe la Dunia mwaka wa 2018.

“Tuna imani ataimarisha matokeo ya timu na kutokana na marufuku ya kutowasajili wachezaji yanayoendelea kutukabili, ni fursa nzuri kwa wachezaji chipukizi kudhihirisha makali yao. Sasa tupo tayari kucheza mechi ya kwanza ya ligi,” akaongeza.