• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:46 PM
Giroud asaidia Chelsea kulaza Rennes na kusonga mbele katika UEFA

Giroud asaidia Chelsea kulaza Rennes na kusonga mbele katika UEFA

Na MASHIRIKA

CHELSEA walitinga hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) wakisalia na mechi mbili zaidi katika hatua ya makundi baada ya fowadi Olivier Giroud kuwafungia bao la dakika ya mwisho katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Rennes ya Ufaransa mnamo Novemba 24, 2020.

Ingawa Giroud ambaye ni raia wa Ufaransa amewajibishwa uwanjani kwa dakika 127 pekee hadi kufikia sasa msimu huu, ushawishi wake umehisika pakubwa na alitegemewa zaidi dhidi ya Rennes baada ya mshambuliaji Timo Werner kupata jeraha.

Daki sita kabla ya Giroud kufunga, Rennes walikuwa wamepania kuwalazimishia Chelsea sare ya 1-1 baada ya Serhou Guirassy kufunga kwa kicha na kusawazisha bao lililokuwa limepachikwa wavuni na chipukiz Callum Hudson-Odoi katika dakika ya 22.

Chini ya kocha Frank Lampard, Chelsea walimiliki asilimia kubwa ya mpira na kutamalaki mchezo huku ushirikiano mkubwa kati ya Hudson-Odoi na Mason Mount ukiwatatiza sana mabeki wa Rennes.

Mechi hiyo iliwapa Chelsea jukwaa la kumkaribisha kikosini beki Thiago Silva huku kipa Edouard Mendy akifanya kazi ya ziada ya kupangua makombora mazito aliyoelekezewa na mafowadi wa Rennes.

Ushindi wa 2-1 uliosajiliwa pia na Sevilla dhidi ya Krasnodar nchini Urusi una maana kwamba mabingwa hao hao wa Europa League wanajivunia sasa alama 10 sawa na Chelsea kileleni mwa Kundi E. Ni pengo la alama tisa ndilo linalowatenganisha wawili hao na Rennes na Krasnodar wanaovuta mkia.

Chelsea kwa sasa wamesalia na michuano miwili zaidi dhidi ya Sevilla na Krasnodar. Kufuzu kwao ni nafuu zaidi hasa ikizingatiwa ugumu wa ratiba yao kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) dhidi ya Tottenham Hotspur, Leeds United na Everton katika jumla ya michuano minane tofauti ya mwezi Disemba, 2020.

Ushindi kwa Chelsea dhidi ya Sevilla ya kocha Julen Lopetegui ugenini utawarahisishia kibarua cha kuvaana na Krasnodar katika mechi ya mwisho. Sevilla waliwalazimishai Chelsea sare tasa katika mchuano wa mkondo wa kwanza uliowakutanisha ugani Stamford Bridge mnamo Oktoba 20, 2020.

Rennes wameshinda mchuano mmoja pekee kati ya 11 iliyopita kwenye soka ya bara Ulaya baada ya kupoteza mara nane na kuambulia sare mara mbili.

Kwa upande wao, Chelsea wamefuzu kwa hatua ya 16-bora ya UEFA mara 16 katika kipindi cha misimu 17 iliyopita. Ni mnamo 2012-13 pekee ambapo Chelsea walishindwa kusonga mbele zaidi katika michuano hiyo baada ya kudenguliwa kwenye hatua ya makundi.

Chelsea wameshinda mechi tatu mfululizo zilizopita za UEFA kwa mara ya kwanza tangu Disemba 2015 na hawajapoteza mchuano wowote kati ya 13 iliyopita katika mashindano yote. Hicho ndicho kipindi kirefu zaidi ambapo hawajapoteza mechi tangu Novemba 2018.

  • Tags

You can share this post!

Uchomaji makaa Boni ungali tishio kwa uhifadhi wa mazingira

Mchakato wa kupata saini za BBI wang’oa nanga