Michezo

Githurai Allstars na MASA watisha Super 8

April 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na JOHN KIMWERE

MECHI za kuwania taji la Super Eight Premier League (S8PL) zilizotinga raundi ya saba wikendi ziliendelea kuchacha huku MASA, Githurai Allstars na Makadara Junior League SA kila moja ikilima mpinzani na kutwaa alama tatu muhimu.

Githurai Allstars ilionekana kivingine ilipocharaza Huruma Kona kwa magoli 5-0 na kwenye patashika iliyosakatiwa uwanjani Stima Club, Nairobi.

Mafanikio hayo yaliipiga jeki kusonga mbele hatua tatu na kutua mbili bora kwa kukusanya alama 13. Nao wanasoka wa Rongai Allstars waliangukia pua walipozabwa kwa maba 3-1 na MASA kwenye mchezo wa kusisimua uliyoandaliwa uwanja wa Makongeni.

Katika uwanja wa Drive Inn, Erick Kariuki alipiga kombora moja safi na kubeba Makadara Junior League SA kukomoa Metro Sports kwa bao 1-0 wiki moja baada ya kulizwa kipigo kama hicho na Mathare Flames awali ikifahamika kama Zamalek FC ambayo hutiwa makali na kocha, Julius Mitivo.

Mashabiki wa MASA walionyesha furaha tele huku wakishangilia kwa nyimbo baada ya timu hiyo kuzoa ushindi wa tatu mfululizo. MASA ilipata ushindi huo baada ya Chris Oduor kuifungia mabao mawili naye Gona Abdalla kuitingia bao moja.

”Ushindi wetu ni zawadi kwa pasaka kwa wafuasi wetu hasa kutoka maandalizi mazuri ya kikosi chetu,” kocha wa MASA, Hosea Akala alisema na kuongeza kuwa hawezi kuficha furaha yake maana vijana wake kushusha mechi mzuri na kuvuna matokeo ya kuridhisha.

Rongai Allstars ilipata bao la kufuta machozi lilijazwa kimiani na Samuel Kapen. Kwenye msimamo wa kipute hicho, mabingwa watetezi Jericho Allstars ingali kifua mbele kwa alama 15, tatu mbele ya Githurai Allstars. NYSA imefunga tatu bora kwa alama 11 sawa na Mathare Flames tofauti ikiwa idadi ya mabao.

MATOKEO KAMILI

Metro Sports 0-1 Makadara Junior League SA.

NYSA 0-0 Mathare Flames

Githurai Allstars 5-0 Huruma kona

Team Umeme 0-0 Melta Kabiria

MASA 3-1 Rongai Allstars