Michezo

Gor kukesha Morocco wakisubiri kutua Algeria

August 27th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na Geoffrey Anene

MABINGWA wa Kenya, Gor Mahia, watakesha nchini Morocco Jumatatu kabla ya kuendelea na safari ya kuenda Algeria kwa mechi muhimu ya Kombe la Mashirikisho la Afrika dhidi ya USM Alger hapo Agosti 29, 2018.

Vijana wa kocha Dylan Kerr waliondoka katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi saa kumi na mbili na nusu asubuhi Agosti 27 na kutua salama salmini nchini Morocco saa nane alasiri saa ya Kenya.

Gor italala nchini Morocco kabla ya kuendelea na safari ya kuelekea Algeria saa sita mchana Jumanne.

Gor inaongoza Kundi D kwa alama nane. Imefunga mabao mengi kuliko nambari mbili Alger, ambayo pia imezoa alama nane. Timu hizi mbili zilijiweka katika hali ngumu zilipopigwa Agosti 19.

Gor ilizabwa 2-1 na Rayon Sports ya Rwanda uwanjani Kasarani nayo Alger ikakubali kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Young Africans jijini Dar es Salaam, Tanzania. Vichapo hivi vilirejesha Rayon katika mbio za kuwania tiketi mbili zilizoko mezani za kusonga mbele.

Rayon ina alama sita. Itafuzu ikipata ushindi dhidi ya Young Africans jijini Kigali kesho nayo Gor ama Alger ipoteze. Hali hii inaweka Gor katika ulazima wa kushinda wenyeji wao ili kujihakikishia nafasi katika mduara wa nane-bora. Gor na Alger ziliumiza nyasi bure zilipokutana katika mechi ya mkondo wa kwanza uwanjani Kasarani mnamo Mei 16.

Timu hizi zilipata motisha kabla ya kumenyana kesho baada ya kushinda mechi zao za ligi hapo Agosti 25. Gor, ambayo inanolewa na Muingereza Dylan Kerr, iliaibisha mahasimu wao wa tangu jadi Leopards 2-0 nayo Alger ilipepeta Hussein Dey 1-0.

Kikosi cha Gor Mahia: Wachezaji – Bonface Oluoch, Fredrick Odhiambo, Haron Shakava, Joash Onyango, Wesley Onguso, Karim Nzigyimana, Ernest Wendo, Humphrey Mieno, Bernard Ondiek, Lawrence Juma, Francis Kahata, George Odhiambo, Samuel Onyango, Jacques Tuyisenge, Francis Mustapha, Charles Momanyi na Philemon Otieno; Maafisa – Dylan Kerr (Kocha Mkuu), Zedekiah Otieno (Naibu Kocha), Jolawi Obondo (Meneja wa timu) na Lordvick Aduda (Afisa Mkuu Mtendaji).