Michezo

Gor Mahia hatujakata tamaa, asisitiza Polack

October 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CECIL ODONGO

KOCHA wa Gor Mahia Steve Polack ni mwenye wingi wa matumaini kwamba klabu hiyo itashinda mechi ya ugenini ya Kombe la Mashirikisho Afrika (CAF) dhidi ya DC Motema Pembe Jumapili hii licha ya kusajili sare ya 1-1 wikendi.

Mwingereza huyu aliwasifia wachezaji wake kwa kung’aa kwenye mchuano huo japo akakiri kwamba walikosa nafasi nzuri za kufunga mabao mengi na kumaliza kazi nyumbani.

“Kulingana na tathmini yangu, wachezaji wengi walitandaza kabumbu safi licha ya kwamba hatukupata ushindi. Mimi ni kocha ambaye hakati tamaa na ninawahakikishia mashabiki kuwa ngoma hii bado itarindimwa hadi dakika ya 90 ugenini. Tuna matumaini ya kusonga mbele kwa kuwa tunahitaji ushindi tu,” akasema Polack kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Katika mechi hiyo ya Jumapili, K’Ogalo walitangulia kufunga kupitia mshambulizi Yikpe Gnamien huku Motema Pembe ikifungiwa bao la pekee na Wiliam Luezi.

Licha ya mlinzi Charles Momanyi kupokezwa kadi nyekundu, mnyakaji wa K’Ogalo David Mapigano alinyaka penalti ya Bongonga Vinny zikiwa zimesalia dakika 10 mechi ikamilike.

Wachezaji walio fiti

Polack pia aliwajibu mashabiki wa K’Ogalo wanaomlaumu kwa kuwapanga nahodha Kenneth Muguna na naibu wake Joash Onyango akisema kuwa sasa K’Ogalo ina wachezaji 16 pekee walio fiti.

“Naelewa shinikizo za mashabiki ila lazima pia nitumie wachezaji ambao ninao. Nilimchezesha Muguna kwa sababu Wendo amekuwa nje kutokana na majeraha na ndiyo alikuwa akirejea timuni. Mimi ndiye huwa nafanya mazoezi na wachezaji hao na ninaelewa hali yao,” akaongeza Polack.

Aidha, alieleza kwamba hatishwi na taarifa zinazozagaa kwamba K’Ogalo itakabiliwa na mapokezi mabaya nchini DRC kutokana na uhasama na hisia kali inayozingira mechi hiyo ya marudiano.

“Nimefanya kazi na timu mbili nchini DRC na ninafahamu tabia zao. Nimeeleza wachezaji wangu wamakinikie tu soka na masuala yote waachie maafisa wa usalama na CAF Jumapili,” akasema.