Michezo

Gor Mahia itaweza kulipiza kisasi kwa USM Alger?

September 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na JOHN ASHIHUNDU

GOR Mahia wamejiandaa kubadilisha matokeo ya mechi ya mkondo wa kwanza dhidi ya USM Alger; timu hizo zitakaporudiana Jumapili ugani MISC Kasarani, lakini wapinzani wao hao kutoka Algeria wamewaonya wasitarajie mteremko.

Mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) walianza mkondo wa kwanza kwa kushindwa 4-1 ugenini, lakini wanatarajiwa kuwa makini mbele ya mashabiki wao wa nyumbani ambao wanatarajiwa kumiminika uwanjani humo kwa wingi.

Gor Mahia wamekuwa wakiandikisha matokeo mazuri nyumbani katika michuano hii ya kuwania ubingwa wa Klabu Bingwa barani Ulaya, tangu washindwe na CNaPS Sport ya Madagascar mnamo 2016. Katika mahojiano ya moja kwa moja na kocha wao, Steven Polack alisema kikosi chake kimejiandaa kufunga mabao ya kutosha na kuweka mfukoni pointi zote tatu.

“Tayari tumejirekebisha na sasa tuko tayari kabisa kuzua upinzani mkali baada ya kujifunza mengi kutokana na mechi ya mkondo wa kwanza. Maandalizi yamekuwa mazuri, licha ya matatizo ya kifedha yanayotukumba kwa sasa,” aliongeza.

Alipoulizwa kuhusu hali ya wachezaji wake walio kambini kwa sasa, Polack alisema kila mtu yuko tayari kwa pambano la Jumapili litakaloanza saa kumi baada ya kushindwa ugenini.

Akizungumza kuhusu mechi hiyo, nahodha wa K’Ogalo Kenneth Muguna amesisitiza kwamba wachezaji wako tayari kupigania ushindi.

“Tunakumbwa na matatizo ya kifedha, lakini hayataathiri kikosi,” alisema.

Gor wamelazimika kutoa namba itakayotumiwa na mashabiki wao kuwatumia chochote walicho nacho baada ya wafadhili wao, SportPesa kujiondoa ghafla kutokana na mvutano wao na Serikali.