• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:12 PM
Gor Mahia kusalia na taji la Ligi Kuu baada ya SDT kufutilia mbali kesi ya KPL

Gor Mahia kusalia na taji la Ligi Kuu baada ya SDT kufutilia mbali kesi ya KPL

Na CHRIS ADUNGO

JOPO la Mizozo ya Spoti (SDT) limetupilia mbali kesi iliyowasilishwa na kampuni ya KPL inayoendesha Ligi Kuu ya Kenya ikipinga maamuzi ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) kutamatisha ghafla kampeni za msimu wa 2019-20 na kutawaza Gor Mahia mabingwa.

Katika maamuzi yake, John Ohaga ambaye ni Mwenyekiti wa SDT, alisema kwamba Afisa Mkuu wa KPL Jack Oguda hakutalii mbinu zote nyinginezo za kutafuta suluhu kati ya KPL na FKF kabla ya kushtaki shirikisho kwa SDT.

Ohaga pia aliamua kwamba Oguda, ambaye alikuwa mlalamishi katika kesi hiyo, aliwasilisha mashtaka bila ya kuwa na idhini kutoka kwa vikosi vya Ligi Kuu ya soka ya humu nchini.

“Hakukuwepo na mwafaka wowote kati ya wadau wakuu wa KPL kabla ya kuwasilishwa kwa kesi hii. Ina maana kwamba mlalamishi alishtaki FKF bila kupata idhini ya kufanya hivyo kutoka kwa wadau wa KPL. Kesi hii kwa hivyo haina mashiko yoyote,” akasema Ohaga.

SDT pia ilisisitiza kuwa maamuzi ya kutamatishwa kwa kipute cha KPL yalichochewa zaidi na mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19 ambao pia ulifanya serikali kupiga marufuku mikusanyiko yote ya umma na kusitisha shughuli zote za michezo ili kukabiliana vilivyo na janga hilo.

Ingawa hivyo, Ohaga pia alisema Rais wa FKF, Nick Mwendwa alikosea kutangaza kutamatika kwa msimu wa KPL 2019-20 kwa kuwa hana mamlaka ya kufanya hivyo baada ya kipindi cha kuhudumu kwa Kamati Kuu ya Kitaifa ya FKF (NEC) kukamilika rasmi mnamo Februari 2020.

“Rais wa FKF si kiwakilishi cha NEC. Kwa sababu hiyo, hakuwa na mamlaka ya kutamatisha Ligi Kuu ya KPL na kutawaza Gor Mahia mabingwa. Ni Baraza Kuu la KPL pekee ndilo lenye uwezo wa kufanya hivyo. Kwa sasa Rais wa FKF ni mfalme asiye na taji la kutambua uongozi wake,” akasema Ohaga.

Mnamo Aprili 30, Mwendwa alitumia mtandao wake wa Twitter kutangaza kuwa mashindano yote ya soka ya humu nchini, ikiwemo Ligi Kuu ya KPL yalikuwa yamefutiliwa mbali kwa sababu ya corona.

SDT pia ilifutilia mbali kesi ya Oguda ya kutaka FKF ifidie hasara ambayo KPL ilikadiria baada ya Mwendwa kutangaza kutamatika rasmi kwa soka ya humu nchini.

Maamuzi ya SDT yanatamatisha sasa uhusiano mbaya wa miaka minne ambao umetamalaki KPL na FKF katika uendeshaji wa soka ya humu nchini. FKF imesisitiza kwamba haitarefusha kipindi cha kuhudumu kwa KPL katika soka ya humu nchini baada ya mkataba wa kampuni hiyo kutamatika rasmi mnamo Septemba 24.

Gor Mahia kwa sasa wana idhini ya kuwakilisha Kenya kwenye soka ya Klabu Bingwa barani Afrika (CAF Champions League) msimu ujao wa 2020-21 baada ya kutawazwa mabingwa wa KPL 2019-20. Taji hilo lilikuwa la 19 kwa Gor Mahia kutia kapuni katika Ligi Kuu ya Kenya.

Mwisho wa uhusiano kati ya FKF na KPL kwa sasa unatarajiwa kutoa fursa kwa shirikisho kusimamia uendeshaji wa Ligi Kuu ya humu nchini kwa udhamini wa kampuni ya mchezo wa kamari ya BetKing kutoka Nigeria. Ligi hiyo itaitwa sasa FKF BetKing Premier League (FKFPL) kuanzia msimu wa 2020-21.

  • Tags

You can share this post!

Mama aliyejitolea kukinga jamii dhidi ya maambukizi ya...

Farah kukosa mbio za mita 5,000 katika Olimpiki za Tokyo