Gor Mahia kutafuta kocha mpya kujaza pengo la Polack
Na CHRIS ADUNGO
GOR Mahia wameagana rasmi na kocha Steven Polack baada ya kuwa naye kwa kipindi cha msimu mmoja pekee.
Mkufunzi huyo raia wa Uingereza ambaye amewaarifu Gor Mahia kupitia barua kwamba amejiuzulu, alijiunga na mabingwa hao mara 19 wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) mwanzoni mwa msimu wa 2019-20.
“Tunathibitisha kupokea barua ya kujiuzulu kwako ambayo iliandikwa Oktoba 8, 2020. Tunasikitikia maamuzi hayo japo tunaheshimu hatua hiyo uliyoichukua. Tunakushuruku kwa kipindi chote ambacho umekuwa nasi na tunajivunia huduma zako za ukufunzi,” ikasema sehemu ya taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Gor Mahia, Samuel Ochola.
“Muda wako nasi ulikuwa wa kujivuniwa na mchango wako ulikuwa mkubwa katika ushindi wa taji la KPL ambalo Gor Mahi walijinyakulia mwishoni mwa msimu wa 2019-20. Tulitamani sana usalie kikosi kwa muda mrefu zaidi kwa sababu ulikuwa kipenzi cha wachezaji na mashabiki wetu,” ikaendelea taarifa hiyo.
Polack alijiunga na Gor Mahia mnamo Agosti 2019 na akawashindia pia miamba hao wa soka ya humu nchini taji la KPL Super Cup. Kuajiriwa kwake kulichochewa na haja ya kujaza pengo la kocha Hassan Oktay ambaye pia aliondoka Gor kushughulikia familia yake nchini Uturuki na akajiuzulu akiwa kwao nyumbani.
Gor Mahia kwa sasa wanajiandaa kwa msimu ujao katika mapambano mbalimbali ya humu nchini na soka ya Klabu Bingwa barani Afrika (CAF Champions League). Mazoezi ya kikosi hicho yanasimamiwa na aliyekuwa msaidizi wa Polack, Patrick Odhiambo.
Mnamo Oktoba 1, 2020, Gor Mahia walitishia kuajiri kocha mpya iwapo Polack asingerejea humu nchini kufikia Oktoba 4, 2020.
Polack aliondoka humu nchini mnamo Agosti na kuelekea Finland kwa likizo ya siku 10 huku akiahidi kurejea na kusaidia Gor Mahia kupiga hatua zaidi kwenye mashindano ya CAF katika kampeni za 2020-21.
Mhazini wa Gor Mahia, Dolfina Odhiambo amefichua sasa mpango wa kuanza kupekuapekua wasifu-kazi wa baadhi ya wakufunzi waliowahi kutuma maombi ya kutaka kupokezwa mikoba ya Gor Mahia hapo awali.
“Hatukushangazwa na maamuzi ya kujiuzulu kwa Polack. Tumehuhudia visa ambapo wakufunzi wa Gor Mahia wanatumia visingizio vya kuenda makwao kwa likizo kisha wakakosa kabisa kurejea,” akatanguliza Odhiambo.
“Ilifikia wakati fulani ambapo tulianza kushuku kwamba Polack asingerejea. Alitazamiwa kurudi pindi baada ya kutamatika kwa likizo aliyoiomba. Hata hivyo, alianza kutumia visingizio vya corona kwamba alitiwa kwenye karantini kwa siku 14 alipowasili Finland,” akasema Odhiambo.